Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balinya amenikumbusha hadithi ya Steven Bengo

Muktasari:

Wanaamini Balinya ni mchezaji wa kiwango cha juu na mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu na kitendo cha kuibuka mfungaji bora wa ligi ya Uganda msimu uliopita kinawafanya waamini kuwa asingeweza kuchemka ndani ya Yanga ukizingatia ni klabu kubwa na inayoweza kumpatia huduma stahiki mchezaji.

Juma Balinya ni mchezaji mwenye jina kubwa hapa Kampala Uganda hasa baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda msimu uliopita wa 2018/2019.

Waganda wanampenda na taarifa za mkataba wake na Yanga kuvunjika juzi kwa makubaliano binafsi zimewasikitisha idadi kubwa ya mashabiki wa mpira wa miguu nchini hapa na wamezipokea kwa majonzi.

Wengi wameshangazwa na taarifa hizo za Balinya kuvunjiana mkataba na Yanga na wanaonyesha kushtushwa nazo kwa sababu kadhaa.

Kwanza mkataba huo umevunjika wakati Balinya hajatimiza hata miezi sita tangu aliposajiliwa mwezi Agosti na alibakiza takribani mwaka mmoja na miezi saba ili mkataba huo umalizike lakini umeishia njiani ghafla akiwa hajatimiza hata nusu ya muda waliokubaliana.

Lakini pili wanashindwa kuelewa imekuaje hadi Balinya ameshindwa kung’aa tangu alipojiunga Yanga hali iliyosabisha klabu hiyo ikubali kirahisi maombi yake ya kuvunja mkataba kama alivyowasilisha mezani.

Wanaamini Balinya ni mchezaji wa kiwango cha juu na mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu na kitendo cha kuibuka mfungaji bora wa ligi ya Uganda msimu uliopita kinawafanya waamini kuwa asingeweza kuchemka ndani ya Yanga ukizingatia ni klabu kubwa na inayoweza kumpatia huduma stahiki mchezaji.

Hata hivyo mambo yamekwenda kombo na mwisho wa siku, mchezaji huyo amekusanya virago vyake na kurejea kwao Uganda kujaribu bahati yake. Kuna sababu kadhaa ambazo pengine zimechangia kumuangusha Balinya hadi akashindwa kuwa na maisha marefu ndani ya kikosi cha Yanga.

Moja ni majeruhi ambayo amekuwa akikumbana nayo tangu alipojiunga na timu hiyo yaliyopelekea akose muda wa kutosha wa kujifua na kujiweka fiti ili aweze kuwa na kiwango kile ambacho alionyesha katika ligi ya Uganda.

Muda ambao mwili ulipaswa kuchanganya kutokana na maandalizi ya mwanzoni mwa msimu, kwa Balinya ndio alikuwa anautumia kujifua ili aweze kuimarika akitokea kwenye majeruhi na kutafuta ufiti wa mechi.

Lakini changamoto nyingine ambayo inaweza kuwa imemgharimu Balinya ni athari ya kisaikolojia kutokana na namna alivyosajiliwa na klabu hiyo wakati wa dirisha la usajili.

Ni mchezaji ambaye Yanga ilitumia nguvu kubwa kumsajili na kumnadi huku ikiweka matumaini makubwa kwake jambo ambalo pengine limechangia kumfanya Balinya awe na presha kubwa ya kutimiza kile ambacho wengi walikitarajia kwake hali inayomfanya akose utulivu na asiwe sawa kisaikolojia.

Pamoja na hayo, inaonekana pia Balinya alikuwa anapata wakati mgumu kuingia na kuzoea staili ya kiuchezaji ya Yanga jambo ambalo lilipunguza ufanisi wake ndani ya uwanja. Akiwa Uganda mara kwa mara alikuwa anapangwa nafasi ya namba kumi au tisa ambayo ilimfanya awe na uhuru na kucheza karibu na lango la adui, jambo lililomwezesha afunge idadi kubwa ya mabao.

Hata hivyo ndani ya Yanga, mara kwa mara amekuwa akichezeshwa nafasi ya mshambuliaji wa pembeni ambayo kwanza inamfanya awe mbali na lango lakini pia si aina ya mchezaji ambaye ana kasi kubwa kuendana na mahitaji ya Yanga kwa upande huo. Inavyoonekana Yanga walimsajili baada ya kuridhishwa na takwimu zake za ufungaji pasipo kumfuatilia kwa ukaribu kama anaendana au haendani na staili yao ya uchezaji.

Hii inanikumbusha pindi Yanga ilipomsajili raia mwingine wa Uganda, Steven Bengo ambaye licha ya kufanya vyema nchini mwao na katika timu yao ya taifa, alishindwa kumudu aina ya soka la Yanga na kujikuta akichemka mapema na kufungashiwa virago vyake.

Kutozaa matunda kwa usajili wa Balinya na Bengo ndani ya kikosi cha Yanga kwa nyakati tofauti ni fundisho kwa klabu zetu kuwa zizingatie mahitaji ya msingi ya timu kabla hazijamsajili mchezaji na ni lazima wajiridhishe kwa vitu vingi kama vile afya yake, tabia na mienendo yake nje na ndani ya uwanja lakini pia kama anaweza kumudu au kutomudu staili na mazingira ya timu pindi akisajiliwa.

Sio kila mchezaji anayefanya vizuri mahali anaweza kufanya vizuri kwingine. Historia ya Steven Bengo na Juma Balinya ni uthibitisho tosha wa hilo.