Championship ni vita ya wababe 'TOP FOUR'

Muktasari:

  • Hadi sasa baada ya kuchezwa michezo 22 kwa kila timu, KenGold inaongoza ikiwa na pointi 50 ikifuatiwa na Biashara United ya Mara yenye pointi 49, wakati Pamba Jiji iko nafasi ya tatu na pointi 47 huku Mbeya Kwanza ikiwa ya nne na pointi 45.

Wakati Ligi ya Championship ikisimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), vita imehamia kwa vigogo wanaoshika nafasi nne za juu kuwania nafasi mbili za kupanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja kwa msimu ujao.


Hadi sasa baada ya kuchezwa michezo 22 kwa kila timu, KenGold inaongoza ikiwa na pointi 50 ikifuatiwa na Biashara United ya Mara yenye pointi 49, wakati Pamba Jiji iko nafasi ya tatu na pointi 47 huku Mbeya Kwanza ikiwa ya nne na pointi 45.


Timu mbili ndizo zitakazopanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja huku zitakazoshika nafasi ya tatu na nne zitacheza ‘play-off’ (mtoano) na mshindi atakayepatikana atakutana na atakayefungwa wa Ligi Kuu Bara kati ya atakayemaliza nafasi ya 13 na 14.


Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Michael Mnyali ‘Chuji’ alisema kwa sasa ligi imefikia sehemu nzuri na hakuna mwenye uhakika wa kupanda.


“Sisi hatujakata tamaa kwa sababu tunaendelea kupambana katika kila mchezo tunaocheza kwa sasa ili tufikie malengo yetu tuliyojiwekea, tunawaandaa wachezaji kuanzia kuwatengeneza kisaikolojia tukitambua bado kazi ni kubwa.”


Kocha Mkuu wa Pamba, Mbwana Makata alisema wanafahamu vita ni kubwa lakini malengo yao msimu huu ni kurudi Ligi Kuu.