Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cheki Selemani Mwalimu alivyovunja rekodi ya Msuva Morocco

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Nyota huyo amecheza Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufanya vizuri kwenye kikosi cha KVZ ya Zanzibar na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2023/2024 akifunga mabao 20 na kutoa pasi za mabao saba (asisti) katika michezo 27 aliyocheza kati ya 30.

MIEZI sita tu ndani ya Ligi Kuu Bara imetosha kumng’oa mshambuliaji wa Singida Black Stars ambaye alikuwa anakipiga Fountain Gate kwa mkopo akimwaga wino kuitumikia Wydad Casablanca ya Morocco.

Si mwingine ni Seleman Mwalimu ‘Gomez’ ambaye amesaini mkataba wa miaka minne na nusu kuitumikia Wydad inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco huku akiweka rekodi mpya ya usajili akimfunika Simon Msuva.

Nyota huyo amecheza Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufanya vizuri kwenye kikosi cha KVZ ya Zanzibar na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2023/2024 akifunga mabao 20 na kutoa pasi za mabao saba (asisti) katika michezo 27 aliyocheza kati ya 30.

Gomez mwenye mabao sita ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu akizidiwa mawili pekee na Elvis Rupia wa Singida Black Stars aliyefunga manane akiwa kinara, amesajiliwa na Wydad kwa ada ya uhamisho ya Sh891 milioni na mshahara wake kwa mwezi ukitajwa kufikia Sh6 milioni, huku kukiwa na bonasi kila akifunga bao.

Kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kulinganisha na Msuva wakati anatoka Yanga kwenda Difaâ El Jadida ya Morocco Julai 29, 2017 kisha Wydad Novemba 10, 2020. Hata hivyo, wakati wa usajili wa Msuva na sasa ni tofauti kwani kipindi hiki klabu nyingi zimekuwa zikimwaga sana fedha kulingana na soko lilivyo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mshambuliaji huyo kinda mwenye umri wa miaka 19, taarifa kutoka Morocco zinabainisha kuwa amesajiliwa na Wydad kwenye kikosi cha timu ya vijana huku akiwa pia na nafasi ya kucheza timu ya kikosi cha kwanza.

ISHU YA MSUVA

Aliyekuwa winga wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anakipiga Al-Talaba SC ya Iraq, Simon Msuva wakati anatua Morocco katika kikosi cha Difaa Hassani El-Jadida Julai 29, 2017, ada yake ya uhamisho ilitajwa kuwa ni Sh173 milioni.

Baada ya kucheza hapo kwa misimu mitatu, Novemba 10, 2020 akahamia Wydad huku usajili wake ukigharimu Sh745.6 milioni.

Hata hivyo, usajili wa Gomez umefunika sajili mbili za Msuva nchini Morocco kwani thamani yake ni Sh891 milioni, akiwa juu kwa wachezaji wazawa waliosajiliwa moja kwa moja kutoka Ligi Kuu Bara kwenda kucheza soka nje ya nchi.

MBWANA SAMATTA

Kabla ya Gomez na Msuva, Mbwana Samatta alikuwa mchezaji wa kwanza mzawa kuuzwa gharama kubwa moja kwa moja kutoka Ligi Kuu Bara wakati akiitumikia Simba na kutua TP Mazembe kwa dau la Sh250 milioni. Ilikuwa mwaka 2011.

Baadae Samatta aliuzwa kwa Sh2.1 bilioni mwaka 2016 kwenda KRC Genk ya Ubelgiji, ambapo pia Januari 2020 akauzwa kwenda Aston Villa ya Ligi Kuu England kwa Sh26 bilioni.

SINGIDA NYOTA WAWILI BILIONI 3

Baada ya dili la Gomez kujiunga na Wydad kwa dau hilo kukamilika, ni wazi Singida Black Stars imeingiza mkwanja mrefu zaidi kwenye biashara ya kuuza wachezaji wake msimu huu.

Timu hiyo yenye maskani yake mkoani Singida, imefanya biashara kubwa mbili hadi sasa ikianza kumuuza beki, Benjamin Tanimu ambaye Agosti 30, 2024 alitimkia Crawley Town inayoshiriki League One ambayo ni ligi ngazi ya tatu nchini England.

Tanimu aliuzwa kwa dau la zaidi ya Sh2.3 bilioni za Kitanzania. Taarifa iliyotolewa na timu hiyo ilibainisha kuwa makubaliano hayo yalijumuisha ada ya uhamisho ya moja kwa moja na ada za mauzo ya baadaye pamoja na ada za ubora na mafanikio ya mchezaji na timu kwa misimu miwili ijayo.

Mauzo ya Tanimu ambayo ni Sh2.3 bilioni na yale ya Gomez Sh891 milioni, ni wazi Singida Black Stars imeingiza Sh3.1 bilioni kupitia madili hayo mawili msimu huu.

TAKWIMU ZA GOMEZ

2023/24
Timu: KVZ (Zanzibar)
Mabao: 20
Asisti: 7
Mechi: 27

2024/25
Timu: Fountain (mkopo)
Mabao: 6
Asisti: 1