Chipo, Mayanga kazi ipo Sokoine
Muktasari:
- Hata hivyo, wakati Mtibwa Sugar ikitamba kufufukia Sokoine jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City wamesisitiza hawako tayari kupoteza pointi yoyote katika mipango ya kujinusuru kushuka daraja kutokana na matokeo waliyonayo.
Pamoja na kukiri ugumu wa mechi za ugenini, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Yusuph Chipo amesema mchezo dhidi ya Mbeya City kiu yao ni pointi tatu ili kujiimarisha kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, wakati Mtibwa Sugar ikitamba kufufukia Sokoine jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City wamesisitiza hawako tayari kupoteza pointi yoyote katika mipango ya kujinusuru kushuka daraja kutokana na matokeo waliyonayo.
Hadi sasa Mtibwa Sugar hawajaonja pointi tatu za ugenini, ambapo kesho Jumamosi itawakabili City mchezo utakaopigwa saa 8 mchana uwanja wa Sokoine.
Mbeya City inahitaji pointi tatu ili kuendeleza matumaini ya kukwepa kushuka daraja baada ya kukusanya pointi 22 na kuwa nafasi ya 14 huku Mtibwa wakiwa nafasi ya 12 kwa pointi 27.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chipo amekiri ugumu wa mechi za ugenini akieleza kuwa kwa muda wa mapumziko mafupi wameimarisha maeneo yote na kesho watafanya kweli kuondoka na ushindi.
Amesema tatizo lililowakuta ni baadhi ya wachezaji kuwa majeruhi na kwamba kwa sasa wote wamerejea kikosini na matarajio ni kupata pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo.
"Tunajua ugumu wa mchezo huo kwa kuwa wapinzani hawako sehemu nzuri na sisi pia tunahitaji hizo pointi tatu, tumekosa matokeo mazuri ugenini ila kesho tunaweza kufanya vizuri, wachezaji wote wamerejea na wako tayari," amesema Chipo.
Kuhusu timu hiyo kuruhusu wastani wa bao kila mchezo, kocha huyo wa zamani wa Pamba Jiji na Coastal Union, amekiri upungufu katika eneo la beki akibainisha kuwa amelifanyia kazi na kesho anatajia matokeo mazuri.
Naye Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga amesema mchezo huo utakuwa mgumu lakini kwa maandalizi waliyofanya yanawapa morali kutamba kushinda mechi hiyo.
Amesema timu hiyo imeruhusu idadi kubwa ya mabao lakini kwa muda aliokuwa nao mazoezini amesahihisha makosa na kuboresha safu ya ushambuliaji na kuwaomba mashabiki wa City kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwasapoti.
"Tumekuwa na muda mzuri wa kujiandaa tukirekebisha makosa na kuboresha maeneo yote, naamini kwa ari na morali iliyopo kwa sasa tunaenda kushinda kesho, mashabiki wawe na matumaini kwamba timu yao itashinda waje kuisapoti" Amesema Mayanga aliyewahi kuinoa Mtibwa Sugar.