Prime
Dabi ya Kariakoo...Kina Mpanzu, Pacome wazingatie haya

Muktasari:
- Kama zilivyo dabi zote nchini, hili ni pambano la kukamiana na lenye ushindani mkubwa kwani likiwa limebeba ramani ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Dabi ya kesho itapigwa kuanzia saa 1:15 usiku, likiwa ni la 114 kwa Ligi ya Bra tangu mwaka 1965.
Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam litapigwa pambano la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga.
Kama zilivyo dabi zote nchini, hili ni pambano la kukamiana na lenye ushindani mkubwa kwani likiwa limebeba ramani ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Dabi ya kesho itapigwa kuanzia saa 1:15 usiku, likiwa ni la 114 kwa Ligi ya Bra tangu mwaka 1965.
Timu zote zinakutana zikiwa na kiu kubwa ya kushinda mchezo huo, hivyo ni kawaida kutumia nguvu, kucheza kwa kasi na kucheza au kuchezewa faulu. Timu zote zina wachezaji wenye kasi kubwa kama Kibu Denis, Ellie Mpanzu na mabeki wa pembeni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala; kwa upande wa Simba, huku Yanga kukiwa na kina Israel Mwenda, Chadrack Boka, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Clement Mzize, ambao wanapaswa kuwa makini kwa aina ya mechi hiyo.
Kutokana na kukamiana huko haitashangaza kuona mchezaji akipata majeraha ya mapema na kutolewa. Hii ni kwa sababu mchezo wa soka unahusisha kukumbana kimwili.
Kona ya Spoti Dokta leo inatoa ufahamu wa mambo ambayo wachezaji wa timu zote hizo wanahitaji kuzingatia kabla ya mchezo huo ili waweze kulinda utimamu wao wa mwili kuelekea mchezo huo.

WANAJIJERUHI HIVI
Mara nyingi katika dakika 15 za mwanzo ndizo huwa shinikizo kubwa kutokana na maelekezo ya benchi huwa ni kutumia dakika hizo kupata ushindi wa mapema.
Wachezaji wanatumia nguvu nyingi na kasi kubwa katika kukabana hatimaye kukwatuliwa na kupata majeraha.
Kupata majeraha ya mapema kunaweza kuwa ni ishara ya wachezaji hawa kutumika sana mara kwa mara kutokana na umuhimu wao katika kuisaidia timu kupata mafanikio.
Mchezo wa soka huwa una mambo mengi uwanjani ikiwamo kutumia nguvu sana kucheza, hivyo ni kawaida wachezaji wa timu hizi kupata mrundikano wa vijijeraha vya ndani kwa ndani na uchovu.
Mchezaji anaweza kupata majeraha yatokanayo na mchezo katika eneo la miguu yanaweza kutokea kutokana na kukimbia kasi, kugongwa, kujipinda vibaya hasa maeneo ya maungio kama goti na kifundo na kutua vibaya wakati wakuruka.
Inawezekana kupata majeraha ya maungio na misuli inapofanya kazi sana ikiwamo kukakamaa, kupata mkazo, kuchanika au kuvutika kupita kiasi.
Katika mchezo huu unakuwa na ushindani mkubwa kwa wachezaji ni kawaida pia kwa mchezaji pinzani kutumia nguvu kubwa kumkaba mwingine hatimaye kuweza kumjeruhi.
Mchezaji kucheza akiwa bado hajapona vizuri, hii inaweza kuwa moja ya sababu kwani kama jeraha halijapona vizuri ni rahisi kupata majeraha tena kwani eneo hili linakuwa sio timamu.
Wakati wakucheza mchezaji mwenyewe anaweza kutumia nguvu sana wakati wakucheza au kukaba, hii inaweza kuchangia kujijeruhi mwenyewe pasipo kuchezewa faulu ikiwamo kujipinda uelekeo hasi.
Kutokana na mchezo wenyewe kuwa na upinzani mkali, ni kawaida kufanyiwa faulu mbaya na kupata majeraha.
Mwanasoka anapokuwa anategemewa katika timu anaweza kuamua kudanganya kuwa hana maumivu ya mwili na kucheza au akalazimishwa kucheza akiwa ametumia dawa za maumivu.
Mchezaji anaweza kushawishika au kudanganya ili tu apangwe kucheza kikosi cha kwanza jambo ambalo humpatia bonasi ikiwamo ile anayopewa endapo atafunga au kuibuka na ushindi.
Huwa ni kawaida majeraha kutokea katika mechi hii bila sababu ya msingi hii ni kutokana na miili ya wachezaji kushindwa kustahimili kucheza kama mechi itakua ngumu.

KUPUNGUZA MAJERAHA
Soka ni mchezo ambao unahusisha kukabana kimwili, pamoja na mbinu mbalimbali zinatumika kupunguza majeraha lakini ni kawaida kutokea majeraha.
Ili kuepuka majeraha ya mapema wachezaji wanahitajika kupasha mwili moto kwa mazoezI mepesi na mazoezi ya viungo kabla ya kuimgia katika mechi.
Mchezaji ahakikishe kuwa ana shikamana na ushauri wa wataalam wa Afya ikiwamo kutocheza mechi hiyo akiwa na maumivu au kama hajapona majeraha ya awali vizur.
Hakikisha unashikamana na ratiba ya mazoezi, chakula, mapumziko na kulala saa 8-10 kwa usiku mmoja katika eneo tulivu lisilo na kelele na msongamano.
Mchezaji asiyepata muda wa kutosha wakupumzika na kulala anaweza kucheza chini ya kiwango kutokana na mwili kuharibiwa utimamu wake.
Hakikisha unalinda upungufu wa maji mwili kwa kunywa maji na juisi za matunda asili. Angalau kunywa maji lita 2-3 kwa saa 24. Mchezaji mwenye upungufu wa maji anapata majeraha kirahisi ikiwamo kupata tatizo la kubanwa misuli.
Mchezaji pia anaweza kujiongeza kwa kuufanyia mwili huduma ya utomasaji kitabibu (body massage) siku chache kabla ya mechi, hii inasaidia kuondoa uchovu katika misuli na pia kuupa utulivu wa mwili na kiakili.

WALIO KATIKA MFUNGO
Timu hizo zinashuka uwanjani mara baada ya waumini wa kiislamu wakitoka kufuru na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, pia wapo kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na hizi ni mbinu kwa wale walio kwenye mfungo kabla ya kushuka uwanjani.
Ingawa mwili una ustahimilivu wa kipekee katika kukabiliana na hali ngumu inazokutana nazo, lakini vizuri kujihami ili mchezaji anayefunga au aliyetoka kufuturu kuingia na kucheza.
Kama ametoka kufuturu basi awe amefuturu mlo mwepesi tepetepe kama uji, supu, viazi na juisi za matunda asili na maji kiasi angalau iwe masaa mawili kabla ya kucheza.
Vyakula viwe na wanga kama vile viazi, ndizi kwani vyakula hivi vinaupa mwili nguvu na wakati juisi au matunda huwa na maji maji na sukari na madini.
Aina hii ya vyakula ni rahisi kunyonywa kwa haraka na mwili hivyo kumsaidia mchezaji kupata nguvu na maji mwilini.
Anayefunga yupo katika hatari ya upungufu wa maji mwilini kutokana na kushinda bila kula wala kunywa kwa muda mrefu hivyo atahitajika kujihami siku 3 kabla ya mechi kula vizuri na kunywa maji mengi
EPUKA KUBOMOA AFYA YA AKILI
Katika kuelekea mchezo huu ni kawaida mashabiki wahamasishaji kucheza na matukio mbalimbali yenye lengo la kuwavuruga kiakili wachezaji ikiwamo kuwapa hofu au kuwatisha na imani za kishirikiana.
Hivyo ni vyema, mchezaji anatakiwa kutulia kambini katika maeneo tulivu yasiyo na usumbufu wa kelele au kuonana na watu wa nje ya kambi yao.
Epuka kufuatilia habari za mitandao ya kijamii ambazo zinaweza kukupa hofu hatimaye kukupa hofu au woga, tatizo ambalo linaweza kuathiri akili hivyo kuondoa kujiamini na umakini wako katika mchezo wa kesho.
Benchi la ufundi linaweza kuwatumia viongozi au wachezaji wa zamani kuja kuwapa hamasa wachezaji na kuwajengea saikolojia nzuri ili kuwafanya wajiamini na kuwa makini uwanjani.
Endapo Mchezaji atabomoka kiakili kabla ya mchezo huo inamweka katika hatari ya kucheza katika kiwango cha chini au kucheza huku akifanya maamuzi mabovu uwanjani au kukosa umakini.