Dickson Ambundo aJiweka sokoni mapema

Muktasari:
- Ambundo alijiunga na Fountain Gate mwanzoni mwa msimu huu akitokea Singida Black Stars amejiengua katika kikosi hicho kwa madai ya kutolipwa malimbikizo ya fedha zikiwamo za usajili zipatazo Sh50 milioni.
WAKATI timu ikipambana kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao, nyota wa Fountain Gate, Dickson Ambundo amefungua milango kwa timu kunasa saini yake akijiengua kikosini.
Ambundo alijiunga na Fountain Gate mwanzoni mwa msimu huu akitokea Singida Black Stars amejiengua katika kikosi hicho kwa madai ya kutolipwa malimbikizo ya fedha zikiwamo za usajili zipatazo Sh50 milioni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwanasheria wa mchezaji huyo, Ali Abdallah alisema ni kweli mchezaji huyo hayupo pamoja na timu kwa madai hayo ya kutolipwa fedha zake za usajili na malalamiko tumeyapeleka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Hawezi kuendelea kuwa pamoja na timu wakati ana madai yake na muda wa umekwisha hivyo kwa timu yoyote inayomuhitaji mchezaji yupo sokoni kwani kwa mujibu wa mkataba, Fountain Gate wameuvunja wao wenyewe,” alisema Ambundo aliyewahi kuwika na Alliance, Gor Mahia ya Kenya, Dodoma Jiji na Singida Big Stars aliyeongeza;
“Baada ya kupeleka malalamiko TFF waliwataka Fountain Gate watulipe madai yetu lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika hivyo kwa maslahi mapana ya mchezaji anaendelea kufanya mazoezi binafsi.”
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha alipotafutwa na Mwanaspoti ili kuthibitisha madai hayo ya Ambundo, alikanusha timu hiyo kudaiwa na kuweka wazi kuwa mchezaji huyo yupo nje ya timu kutokana na kuomba ruhusa ya kujiuguza.
“Taarifa hizo hazina ukweli wowote. Ambundo bado ni mchezaji wetu halali yupo nje ya timu, kwa sababu anaugua na taarifa hiyo ndiyo tuliyonayo kuhusu kuidai klabu ndio kwanza nakusikia wewe,” alisema Tabitha.