Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Inonga aleta kizaazaa Yanga, mabosi wagawanyika

INONGA Pict
INONGA Pict

Muktasari:

  • Wachezaji waliowahi kupita Simba na kutua Yanga kwa miaka ya hivi karibuni walioshindwa kucheza kwa kiwango kikubwa kama ilivyotarajiwa ni pamoja na Jean Baleke, Clatous Chama, Jonas Mkude na Augustine Okrah.

DILI la beki wa kati wa zamani wa Simba anayekipiga FAR Rabat ya Morocco, Henock Inonga kutua Yanga limeibua mvutano mkali baada ya kutokea mgawanyiko kwa mabosi wa klabu hiyo, huku baadhi wakitaka asisajiliwe.

Katika hoja mbili zinazovutana juu ya dili hilo, wanaosema asisajiliwe wanasisitiza kwa sasa hawataki kuona wanamsajili mchezaji ambaye amepita Simba, huku wale waliopendekeza asajiliwe wanasimamia kwenye msimamo wao kwamba ni mchezaji mzuri atawasaidia.

Hivi karibuni, Mwanaspoti lilikujuza kwamba Yanga iko mbioni kufanya makubaliano na Mkongomani huyo aliyewahi kuitumikia Simba kabla ya kutimkia FAR Rabat ya Morocco aliko sasa.

Baada ya kuwepo kwa taarifa hizo, ishu mpya ni kwamba mabosi wa klabu hiyo wamegawanyika, huku wengine wakitaka usajili huo ufanyike na wengine wakigomea.

Mtoa taarifa kutoka ndani ya Yanga, ameliambia Mwanaspoti kuwa: "Baadhi ya mabosi wamechoka mazoea ya kuchukua wachezaji kutoka kwa wapinzani wetu wakubwa wakati mastaa wapo wengi tu.

"Lakini sababu nyingine kubwa ni kuwa mastaa hao wakitua Yanga hawana makali kama walivyodhania, hivyo ni bora kwa sasa kuangalia wachezaji kutoka sehemu nyingine na sio waliopita Simba," kilisema chanzo hicho na kuongeza;

"Wanaopinga wanataka atafutwe beki mwingine, lakini sio Inonga kwani anaweza kuja kufanya makosa ikatafsiriwa ni kwa sababu amewahi kucheza Simba hivyo amekuja kutuhujumu."

Mwanaspoti iliwahi kuandika kuhusu ripoti ya kocha wa timu hiyo, Miloud Hamdi ambaye aliweka wazi kuwa msimu ujao Yanga inahitaji beki, kiungo mkabaji, namba kumi na mshambuliaji wa mwisho.

Lakini inadaiwa, Yanga bado hawajasemehe kilichotokea kwa Inonga, kwani wakati anatua kwa mara ya kwanza nchini msimu wa 2021-2022 pamoja na Fiston Mayele, wote walitakiwa kusaini Yanga, lakini yeye akatimkia Simba.

Rekodi za Inonga kwa msimu huu zinaonyesha katika mechi za hivi karibuni amekuwa akikaa benchini, huku katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akicheza mechi moja tu dhidi ya Pyramids kwa dakika 30.

Wakati hayo yakiendelea, kumekuwa na kawaida ya wachezaji kuhama kutoka Simba kwenda Yanga na kinyume chake huku wapo waliofanikiwa kufanya vizuri na wengine kufeli.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Yanga imefaidika na huduma ya Kelvin Yondani, Athuman Idd 'Chuji', Amissi Tambwe na sasa Israel Mwenda waliofanya vizuri Simba na kutua Yanga wakiendeleza makali yao.

Wachezaji waliowahi kupita Simba na kutua Yanga kwa miaka ya hivi karibuni walioshindwa kucheza kwa kiwango kikubwa kama ilivyotarajiwa ni pamoja na Jean Baleke, Clatous Chama, Jonas Mkude na Augustine Okrah.