Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fainali FA kwa Ouma, Hamdi ni zaidi ya mechi

Muktasari:

  • Hiyo inatokana na yeyote atakayeshinda, ataweka rekodi katika maisha ya ufundishaji ambapo Hamdi anakutana na Singida,  timu iliyomtambulisha Desemba 2024 kuwa kocha wa timu hiyo, kisha akaibukia Yanga Februari 2025 alipo hadi sasa.

KOCHA wa Yanga, Miloud Hamdi na David Ouma wa Singida Black Stars, kila mmoja anaitazama fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kuwa ni zaidi ya mechi.

Hiyo inatokana na yeyote atakayeshinda, ataweka rekodi katika maisha ya ufundishaji ambapo Hamdi anakutana na Singida,  timu iliyomtambulisha Desemba 2024 kuwa kocha wa timu hiyo, kisha akaibukia Yanga Februari 2025 alipo hadi sasa.

Makocha hao leo Juni 28, 2025 wana kazi ya kufanya katika programu za mwisho ya mazoezi yatakayofanyika kwa nyakati tofauti kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kisha kesho Jumapili Juni 29, 2025 kuamua nani mbabe katika mechi hiyo ya fainali ya  itakayochezwa uwanjani hapo saa 2:15 usiku.

Hamdi ambaye leo saa 12 jioni atakuwa na kikosi cha Yanga katika mazoezi ya mwisho, amesema ushindi kwa kesho itamfanya kuweka rekodi ya kutwaa mataji mawili makubwa kwa msimu mmoja ndani ya Yanga kama ilivyofanya timu hiyo msimu uliopita chini ya Miguel Gamondi.

"Fainali hii kwangu inamaanisha tunakwenda kushinda makombe mawili, tayari tumeshinda ligi na sasa tukishinda hii maana yake ni makombe mawili," amesema Hamdi na kuongeza;

"Wachezaji wana uzoefu na hilo kwani wameshinda mataji mawili kwa msimu mara nyingi, lakini nataka kufanya hivyo kesho nikiwa nao.

"Kombe ni sehemu ya mafanikio ya klabu, Yanga ni klabu ya kushinda makombe, hivyo kwangu sio tu kucheza fainali, nipo hapa kwa ajili ya kushinda."

Kwa upande wa Ouma ambaye naye leo saa 2 usiku atakuwa na programu ya mwisho ya mazoezi, amesema kwa kuwa msimu uliopita alishindwa kupenya fainali akiishia nusu fainali alipokuwa Coastal Union na kufungwa 3-0 na Azam, lakini sasa ni wakati wa kuweka rekodi.

"Kwanza nashukuru kuona narudi tena kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, safari hii nikiwa na Singida Black Stars baada ya kufanya hivyo na Coastal Union msimu huu," amesema Ouma raia wa Kenya aliyeongeza;

"Nikiwa Coastal Union, msimu uliopita tuliishia nusu fainali katika Kombe la FA, lakini sasa hapa Singida Black Stars tumeingia fainali.

"Nataka kuona tunashinda kikombe na kuweka historia mpya ndani ya klabu hii.

"Ukiangalia uwekezaji uliowekwa ndani ya klabu, umejengwa uwanja pale Mtipa, itapendeza tukipeleka kombe," amesema Ouma.

Rekodi za Kombe la FA zinaonesha Yanga imetwaa taji hilo mara nne tangu michuano hiyo iliporejea msimu wa 2015-2016, ikiwa ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi ikifuatiwa na Simba (3), Mtibwa Sugar (1) na Azam (1).

Singida haijawahi kutwaa ubingwa wowote tangu ipande daraja kushiriki Ligi Kuu Bara ilipokuwa ikifahamika Ihefu FC kabla ya mwanzo mwa 2024 kuuzwa na kutambulika kwa jina la Singida Black Stars.