Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Geay mzigoni Yangzhou Half Marathon kesho Jumapili

Muktasari:

  • Mbio hizo zitakuwa za tatu mwaka huu kwa mwanariadha huyo kushiriki baada ya kukutana na changamoto za kiafya mwaka 2024.

Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay amesema amejiandaa kushinda mbio za Yangzhou Half Marathoni zitakazofanyika kesho Jumapili Machi 30, 2025.

Mbio hizo zitakuwa za tatu mwaka huu kwa mwanariadha huyo kushiriki baada ya kukutana na changamoto za kiafya mwaka 2024.

Tangu muda huo, alianza na Aramco Huston Half Marathoni za nchini Marekani ambapo alishika nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 59:18.

Muda huo ulimfanya kuvunja na kuweka rekodi mpya ya taifa ya nusu marathoni iliyodumu kwa miaka saba tangu ilipowekwa mwaka 2017 na marehemu Ismail Juma kwa muda wa dakika 59:30 kupitia mbio za nusu marathoni za Jamhuri ya Czech.

Baada ya hapo akashiriki Daegu Marathoni za Korea Kusini ambapo alishika nafasi ya kwanza kwa muda wa saa 2:05:20 na kuweka rekodi ya mwanariadha wa kiume ambaye amekimbia muda mchache zaidi kwenye mbio hizo.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa nchini China, Geay ambaye pia anashikilia rekodi ya marathoni ya taifa kwa muda wa saa 2:03:00, amesema amejiandaa vizuri kupambana na kufanya vyema.

“Natarajia nitakimbia vizuri japo siwezi kusema nitashinda kwani sijui wapinzani wangu wamejiandaa vipi lakini nimefanya maandalizi ya kutosha," amesema Geay.

Ameongeza kama mambo yataenda vizuri jinsi ambavyo amepanga anaamini kesho ataipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa kwa kuongoza na kuwashinda wababe ambao watashiriki mbio hizo.

“Natambua kutakuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wanariadha wengine, ndio maana nimejitahidi kufanya maandalizi ambayo yatanifanya kwenda kushinda kesho,” ameongeza.

Geay ambaye msingi wake imara wa riadha ulijengwa kupitia mbio ndefu za viwanjani mita 5000 na 10000 ameweka wazi kuwa baada ya kumaliza nguvu zote atazielekeza katika mashindano mengine kwani mwaka jana hakufanya vizuri kutokana na majeraha yaliyomkabili.