IAA yabeba ubingwa, yapanda First League

Muktasari:
- "IAA imeongeza idadi za timu za Arusha katika mashindano makubwa ambayo yanasimamiwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kufikia tatu, awali zilikuwa mbili Mbuni na TMA Stars ambazo ziko Championship"
Timu ya Soka ya Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA SC) imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Mikoa RCL 2025 baada ya kuifunga Misitu ya Tanga kwa penalti 4-2 katika mchezo wa fainali baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 2-2.
IAA sasa imeongeza idadi za timu za Arusha katika mashindano makubwa ambayo yanasimamiwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kufikia tatu, awali zilikuwa mbili Mbuni na TMA Stars ambazo ziko Ligi ya Championship na sasa pia IAA ya ambayo imepanda First League.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa leo Ijumaa Mei 2, 2025 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha ambapo dakika 45 za kwanza zilianza kasi huku IAA wakimiliki mchezo kwa asilimia kubwa.
Ambayo iliwafaidisha dakika ya 23 kupitia Jeremia Ephu aliyefunga kwa penalti baada ya kipa wa Misitu kumfanyia madhambi mchezaji wa IAA.
Kipindi cha pili, Misitu walirejea kwa kasi na kuchukua mechi hiyo wakitaka kurekebisha makosa walifanya kipindi cha kwanza lakini kukosa umakini kwa safu ya ushambuliaji na umakini wa mabeki wa IAA .
Iliwachukua hadi dakika ya 90+4 Msitu kuwakatili wakati vijana wa Chuo cha Uhasibu Arusha waliokuwa wanaamini tayari wameshatwaa ubingwa kwa kufunga bao la kusawazisha.
Kwa mujibu wa kanuni ya mashindano ya RCL hatua ya fainali na mshindi wa tatu dakika 90 zikikamilika bila mshindi kupatikana zinaongezwa dakika 30 za ziadi ambapo pia mshindi asipopatikana ndani ya dakika hizo 120 zinapigwa penalti.
Ambapo katika dakika 30 za nyongeza IAA walipata goli mapema tu dakika ya 91 kupitia yule yule Jeremia Ephu ambaye alifunga kupitia mkwaju wa penalti baada ya kip wa Misitu kumchezea madhambi mchezaji wa IAA ndani ya boksi.
Hata hivyo, Misitu haikukata tamaa kwa kuendelea kutafuta bao la kusawazisha ililopata dakika ya 105 kupitia kwa Ismail Mbaga na kufanya dakika 15 za kwanza kukamilika kwa 2-2.
Dakika 15 za pili timu zote zilikuwa zinashambuliana kwa zamu ila ikakosekana ubunifu wa kuweza kubadilisha tena ubao wa matangazo na kufanya dakika 120 za jumla kukamilika kwa sare ya 2-2.
Katika mchezo ambao upigwa mapema saa 7:30 mchana kutafuta mshindi wa tatu,Kajuna FC ya Kigoma lishinda goli 1-0 dhidi ya Cargo FC ya Dar Es Salaam kupitia goli la Ally Ramadhan dakika ya 68.
IAA na Misitu zote zimepanda daraja hadi Ligi ya First League huku Kajuna na Cargo zenyewe zitacheza mchezo wa mtohano (playoff) kupanda dhidi ya timu za First League ambapo kama zitashinda zitapanda hadi First League na zile za First League zitashuka ila kama zitapoteza zibaki mkoani kwa maana ya Ligi daraja la tatu na zile za First League zitabaki pia .