JICHO LA MWEWE: Singano, Ambokile, Kibabage, kama Wanaigeria halisi

Muktasari:
Sijui kwanini hatuanzi kuitumia Genk kama njia. Wakati watu wanasumbuka na Kevin John ‘Mbappe’ huku hatima yake ikiwa haijulikani, ingekuwa rahisi tu kwake kwenda Genk ya vijana na kuanza kufanya makubwa taratibu.
RAMADHANI Singano, aliwahi kuitwa ‘Messi.’ Wiki iliyopita alisaini TP Mazembe ya DR Congo. Ni baada ya kuachwa na Azam FC. Ni baada ya Simba na Yanga kumuona amepitwa na wakati. Hakuna klabu yoyote iliyomtamani kati ya Simba na Yanga.
Ana bahati ya mtende amesaini mkataba mrefu katika klabu kubwa kama ya Mazembe. Kama akiweza kuimarika na kurudi katika makali yake atalisaidia taifa kama ilivyo kwa baadhi ya wachezaji wa nje wanaotubeba kwa sasa.
Sijui ilikuaje akapata dili hilo lakini watu wa ndani wa Mazembe lazima wanawaamini wachezaji wa Kitanzania kwa sasa. Kabla ya hapo mshambuliaji anayeitwa Eliud Ambokile alisaini TP Mazembe. Si unaona sasa. Lazima wanawaamini wachezaji wa Kitanzania.
Na kabla ya hapo TP Mazembe ilikuwa inamtaka mchezaji anayeitwa Ibrahim Ajibu. Dili lake lilivurugwa ovyo na Ajibu mwenyewe lakini bado inawaamini wachezaji wa Tanzania. Kisa? Mambo makubwa ambayo Mbwana Samatta aliyefanya kwao. Na kisha Thomas Ulimwengu.
Congo inaamini mpaka leo kuna Samatta mwingine Tanzania. Haitaacha kuchungulia Tanzania kila madirisha ya uhamisho yanapofunguliwa. Haiamini kama Tanzania ilikuwa na Samatta mmoja tu.
Wenzetu ndivyo walivyo. Akipita mtu mahala akaacha jina kubwa unawafungulia njia wenzako njia. Ndivyo ilivyo. Na imetokea tena kule Morocco katika Klabu ya Difaa Jadida ambayo anachezea mdogo wetu, Saimon Msuva.
Msuva amefungua njia kwa Watanzania kuaminika klabuni pale. Juzi wale jamaa wamemchukua beki wa kushoto wa Mtibwa Sugar na Timu ya Taifa ya Vijana, U-17, Nickson Kibabage. Dili safi kabisa. Kibabage anakwenda kupambana katika upande wa kushoto pale Morocco.
Ukienda Congo au Morocco ukawaambia Watanzania hawajui mpira hawatakuelewa? Ni rahisi tu. Tumeacha alama. Kama ambavyo ukienda Genk au Ubelgiji kwa sasa ukawaambia kuwa Watanzania hawajui mpira, hawatakuamini.
Kwa sasa Genk wanaamini Tanzania lazima kuna Samatta mwingine. Lazima watahisi nchi ya Tanzania haijatumika vema katika kuleta vipaji Ulaya. Wakati mwingine uzuri wa Wazungu wanaweza hata kufungua shule ya soka nchini kwa sababu ya Samatta tu. Wataweka mitego yao hapa kwa ajili ya kuwasaka kina Samatta wengine kwa sababu mpira kwao ni biashara kubwa.
Sijui kwanini hatuanzi kuitumia Genk kama njia. Wakati watu wanasumbuka na Kevin John ‘Mbappe’ huku hatima yake ikiwa haijulikani, ingekuwa rahisi tu kwake kwenda Genk ya vijana na kuanza kufanya makubwa taratibu.
Hivi ndivyo watu wa Afrika Magharibi walivyo. Anapenya mmoja, anafanikiwa kisha wengine wanafuata njia. Inakuwa ama kwa kupelekwa na aliyefanikiwa, au na watu wengine lakini wakitumia mwanya wa uaminifu wa aliyepita.
Wasifu ni kitu kikubwa kwa wachezaji wanaotaka kwenda nje ya nchi. Kwanza kabisa wanalazimika kuwa na wasifu mzuri. Wasifu binafsi. Lakini baada ya hapo wanahitajika kuwa na wasifu wa taifa lao. Taifa lao ni lipi? Taifa lao limewahi kumtoa nani?
Alex Iwobi anacheza Arsenal kwa sababu pale aliwahi kupita Nwankwo Kanu. Lakini pia aliaminika pale kwa sababu ni mtoto wa dada yake staa wa zamani wa Nigeria, Austin Jay Jay Okocha. Wenzetu wanatumia faida hii.
Wachezaji wa Afrika Magharibi wametapakaa Ulaya kwa sababu hii. Sisi tumechelewa lakini sio mbaya tukaanza kutumia safari kwa waliofanikiwa. Niliwahi kumuuliza Rashid Mandawa, kwanini asitoke Botswana na kusogea Afrika Kusini katika klabu ya Abdi Banda, Baroka kwa sababu tayari Banda alikuwa ameaminiwa katika klabu ile kiasi cha kupewa unahodha. Sikupewa majibu ya uhakika.
Wakati mwingine huwa ninasikitika mchezaji wa Tanzania anapokwenda nje ya nchi halafu akaanza kufanya mambo ya ajabu. Anawanyima njia wenzake. Kuna wachezaji kadhaa wa Tanzania tunawafahamu wamefanya mambo ya ajabu nje, kiasi kwamba wachezaji wa Kitanzania hawaaaminiki tena huko.
Kocha mmoja wa Afrika Kusini aliwahi kujiapiza kamwe hatakuja kuchukua tena mchezaji wa Kitanzania. Kisa? Aliwahi kuwa na mchezaji mmoja mzuri wa Kitanzania lakini alikuwa msumbufu. Kila mwezi alikuwa anataka kurudi nyumbani. Nasikia alikuwa ana wake watatu nyumbani Tanzania.
Mchezaji mwingine alikwenda Ulaya akafanya visa vya ajabu ajabu. Sidhani kama klabu yake inaweza kurudia kumchukua mchezaji kutoka Tanzania. Inavyoonekana Watanzania wote tumeonekana wendawazimu mbele ya kocha yule au mabosi wa klabu ile.
Tukirudi kwa kina Singano, Ambokile na Kibabage nadhani wanajua kwanini wameaminiwa kwenda walikokwenda. Walifunguliwa njia nzuri. Wasipokazana wakachemsha marafiki zetu wa hizo klabu wanaweza kudhani kwamba vipaji vya kina Samatta na Msuva vilikuwa vya kubahatisha tu na taifa haliwezi tena kutoa wachezaji wazuri. Huwa inatokea mara nyingi.
Wakakomae tu.