Juma Balinya (JB) rekodi zake zaleta mzuka mpya Yanga

Muktasari:
Shughuli ya JB anayoifanya huko mazoezi tayari imewapa mzuka wachezaji wenzake wakiamini kwamba, nyavu za timu pinzani zitatingishwa sana na kama hili litatokea basi inaweza kuwa pigo kubwa kwa Simba.
Dar es Salaam. MSIMU uliopita kwenye kikosi cha Yanga kulikuwa na mtu mmoja anaitwa Heritier Makambo. Huyu alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Jangwani kutokana na kuifanya vyema kazi yake ya kupasia mipira nyavuni. Yanga haikuwa na nguvu kubwa kuichumi, lakini Makambo alikuwa anawapa tumaini na jeuri ya kubishana na watani zao huko mitaani kutokana na shughuli yake uwanjani na kuiweka Yanga kileleni mwa msimamo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, msimu ujao Yanga haitakuwa na Makambo aliyemaliza na mabao 17 baada ya kutimkia zake Horoya ya Guinea.
Lakini wenyewe Yanga wanakwambia kimetoka kitu kimeingia kitu na msimu ujao kazi hiyo itafanywa na straika mpya aliyenaswa kutoka Police ya Uganda, Juma Balinya a.k.a JB.
JB, ambaye kwa sasa anaendelea kunolewa kwenye kambi ya Wana-Jangwani hao iliyopo kule Bigwa, Morogoro, ndiye Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Uganda na mashabiki wa Yanga ni kama wameanza kumsahau Makambo.
Shughuli ya JB anayoifanya huko mazoezi tayari imewapa mzuka wachezaji wenzake wakiamini kwamba, nyavu za timu pinzani zitatingishwa sana na kama hili litatokea basi inaweza kuwa pigo kubwa kwa Simba.
Awali, JB alikuwepo kwenye orodha ya wachezaji ambao mabosi wa Simba walikabidhiwa na wakala Patrick Gakumba, lakini walimtema wakati huo Yanga wakiwa tayari wameanza mawasiliano ya kunasa huduma yake.
Hapa Mwanaspoti kwa uchache tu linakupa data za JB ili umfahamu kabla ya kuanza cheche zake kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ambayo Yanga itashiriki.
REKODI
19- Mabao aliyofunga katika Ligi Kuu ya Uganda na kubeba tuzo ya Mfungaji Bora
18 Namba ya jezi anayovaa Yanga
1 Idadi ya Hat trick msimu uliopita dhidi ya Black Angels 2018-19 Ilibeba Tuzo ya Mchezaji Bora Uganda
12 Idadi ya mechi ilizofunga msimu uliopita
8 Idadi ya timu alizozifunga
5 Idadi ya pasi za mwsho alizotoa
6 Idadi ya mabao ya aliyofunga ugenini
13 Idadi ya mabao aliyofunga nyumbani