Kaseja azichungulia dakika 180 za kubaki

Muktasari:
- Katika hesabu za kujinasua na janga la kushuka daraja, kocha huyo amesema ana mechi mbili ngumu sawa na dakika 180 dhidi ya Azam na Simba ambazo anaona zimeshikilia hatma yao.
KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja ameshtushwa na mfululizo wa matokeo mabaya ya kikosi chake kilichopoteza mechi mbili mfululizo za ligi huku akikiri mambo yanazidi kuwa magumu kwao.
Katika hesabu za kujinasua na janga la kushuka daraja, kocha huyo amesema ana mechi mbili ngumu sawa na dakika 180 dhidi ya Azam na Simba ambazo anaona zimeshikilia hatma yao.
Kagera Sugar imetoka kupoteza dhidi ya Tanzania Prisons kwa bao 1-0 kisha ikachapwa 2-0 na Dodoma Jiji, mechi zote zimepigwa ugenini na kuifanya timu hiyo kushuka hadi nafasi ya 15 ikikusanya pointi 22.
Kabla ya vipigo hivyo, Kagera ilishinda mechi mbili mfululizo na kuibua matumaini ya kuwa sehemu salama na hatari ya kushuka daraja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaseja amesema mambo yanaendelea kuwa magumu upande wake lakini anaamini bado ana nafasi ya kujenga kikiosi chenye mwendelezo wa matokeo mazuri kwenye mechi nne zilizobaki ambazo amekiri kuwa zimeshikilia hatma ya yeye kuibakiza timu hiyo.
“Kupoteza mechi mbili mfululizo na hatupo nafasi nzuri sio picha nzuri kwetu, tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha timu inabaki ligi kuu, hatutaki kuwa sehemu ya kuandika histori ya kuishusha timu ambayo imehudumu zaidi ya miaka 20 bila kushuka,” alisema na kuongeza.
“Nina kibarua cha kusaka pointi 12 kwenye mechi nne zilizobaki, timu za Simba na Azam FC ambazo zina uhakika wa kucheza ligi hadi muda huu ndio zimeshikilia hatma yangu ya kuipambania Kagera icheze ligi msimu ujao ukiondoa timu nyingine mbili ambazo pia zinapambana kama sisi.”
Kocha huyo ambaye ni kipa wa zamani wa Simba, Yanga, Kagera Sugar na Taifa Stars, amesema ukiondoa Simba na Azam FC, ana mtihani wa kukabiliana na Mashujaa na Namungo.