Kaseke, Ntibazonkiza watakata, Yanga ikiichapa Ihefu

Mchezo wa Ligi Kuu raundi ya 17 uliozikutanisha timu za Ihefu na Yanga umemalizika na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 3-0.
Mchezo huo unakuwa wa mwisho kwa mzunguko wa kwanza kwa Yanga,ulianza kwa timu zote mbili kushambuliana japo Yanga walionekana kuwazidi ubora Ihefu katika kutengeneza mashambulizi na dakika ya 12 walipata bao kupitia kwa Deus Kaseke aliyefunga kwa mguu wa kulia akipokea pasi mpenyezo toka kwa Said Ntibazokiza aliyewatoka mabeki wa Ihefu kwa chenga.

Bao hilo lilionenekana kuwafanya Ihefu kuongeza umakini katika ukabaji wao na walifanikiwa kudhibiti mashambulizi ya Yanga kadha yaliyokuwa langoni kwao kwa dakika 45 za mwanzo.
Dakika ya 43 kocha mkuu wa Ihefu Zuberi Katwila alifanya mabadiliko kwa kumtoa Jeremia Katula na nafasi yake kuchukuliwa na Wiliam Mgaya.
katika mchezo huo kocha mkuu wa Yanga Cedric Kaze aliwaanzisha Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Mustapher Yassin, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tunombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Yacouba Songne, Deus Kaseke na Said Ntibazonkiza.
Ihefu walioanza ni Deogratias Munishi, Mando Mkumbwa, Omary Kindamba, Wema Sadoki, Michael Masinda, Samweli Jackson, Juma Mahadhi, Jeremia Katula, Joseph Kinyozi, Shaban Iddy na Joseph Mahundi.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadaliko Yanga wakiwatoa Tunombe Mukoko na kuingia Zawadi Mauya (45), Said Ntibazonkiza nafasi yake ikichukuliwa na Farid Mussa (58), na Deus kaseke aliyempisha Haruna Niyonzima (76) huku Ihefu akitoka Juma Mahadhi na nafasi yake kuchukuliwa na Andrew Simchimba dakika ya (45).
Dakika ya 49 Yacouba Songne aliwapatia Yanga bao la pili akipokea pasi kutoka kwa Said Ntibazonkiza na dakika ya 59 Feisal Salum 'Feitoto' aligongelea msumari wa mwisho baada ya kupokea pasi kutoka kwa Deus Kaseke na kupiga shuti lililomshinda golikipa wa Ihefu Deogratius Munishi na kuzama nyavuni.
Ushindi huo unawafanya Yanga kumaliza mzunguko wa kwanza bila kupoteza mchezo wowote wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kucheza jumla ya mechi 17 wakishinda mechi 13 na sare nne na kuvuna alama 43.
Ihefu wao wapo nafasi ya pili kutoka mkiani (17) wakiwa wamecheza mechi 17 na kushinda tatu, sare nne na kupoteza 10.