Kifaa kipya Yanga hiki hapa

YANGA inapambana kupata saini ya straika namba moja wa DC Motema Pembe ya DR Congo, Dark Kabangu, Mwanaspoti linajua.
Kama Yanga itafanikiwa kumnasa mchezaji huyo utakuwa usajili wa pili wa Kocha Cedrick Kaze baada ya ule wa Saido Ntibazonkiza wa Burundi ambaye kuanzia leo atakuwa huru kuichezea Yanga. Dirisha dogo la usajili limefunguka usiku wa kuamkia leo huku Saido akiwa mchezaji huru.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata jana kutoka DRC ni kwamba wakala wa Kabangu ndiye anayewasimamia pia Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda na mazungumzo yanaendelea baina ya vigogo wa Yanga ila ugumu upo mmoja tu. Kabangu anataka Yanga imvumilie mpaka baadae mwezi Januari akacheze michuano ya CHAN nchini Cameroon jambo ambalo limeibua sintofahamu. Kabangu amewahi kucheza soka Hungary na Armenia na Yanga walikuwa wakimuwinda tangu mwaka jana ila wakashindwana dau.

Habari zinasema kwamba Yanga wanaendelea kumshawishi straika huyo mzoefu lakini ikishindikana kabisa wiki hii watafanya uamuzi mwingine. Vyombo vya habari vya Kinshasa vimeripoti kwamba Yanga wana uwezekano mkubwa wa kumpata Kabangu mwenye mabao sita msimu huu ingawa Mwanaspoti linajua bado kikwazo ni michuano hiyo ambayo anataka kwenda kucheza aweke rekodi na kuongeza soko lake.
Kaze ameiambia Mwanaspoti wiki hii kwamba; “Nataka straika mmoja wa maana sana, lakini bado napitia rekodi za wachezaji mbalimbali nilionao ndio nifanye uamuzi.” Kocha huyo ambaye ametimiza siku 55 ndani ya Yanga aligoma kuweka wazi majina aliyonayo ingawa mashabiki wameonekana kukubali mafanikio yake na kuwa na shauku ya kujua anayemshusha tena atakuwaje.
Kaze alianza kuinoa rasmi Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania uliochezwa Oktoba 22 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililopachikwa na kiungo Tonombe Mukoko.
Tofauti na matarajio ya wengi ambao waliamini kuwa Kaze angehitaji muda mrefu kuifanya Yanga kuwa tishio katika Ligi Kuu msimu huu, kocha huyo ametumia siku chache kuibeba Yanga.
Ikiwemo matokeo mazuri sambamba na kutopoteza mechi. Kocha huyo aliikuta Yanga ikiwa imecheza mechi tano za Ligi Kuu bila kupoteza, ikishinda nne na kutoka sare moja, ikifunga mabao saba na kufungwa bao moja huku ikiwa na wastani wa kufunga bao 1.17 katika kila mchezo.
Chini ya Kaze, Yanga imecheza mechi 10, ikishinda saba, kutoka sare tatu, ikifumania nyavu mara 15 huku yenyewe ikiruhusu mabao manne.

Dondoo zinadhihirsha kwamba ameimarisha zaidi ulinzi, kuimarisha viwango vya kundi kubwa la wachezaji tofauti na alivyowakuta ambapo baadhi walionekana wangeweza kutupiwa virago katika dirisha dogo.
Mfano wa wachezaji ambao Kaze amewaimarisha vilivyo ni kiungo Deus Kaseke ambaye kwa sasa amekuwa uti wa mgongo wa timu hiyo katikati mwa uwanja katika kuunganisha na kuichezesha timu, kutengeneza nafasi na kufunga mabao muhimu.
Chini ya Kaze, Kaseke ameifungia Yanga jumla ya mabao manne katika Ligi Kuu huku akipiga pasi tatu zilizozaa mabao.
Mchezaji mwingine aliyeimarika vilivyo chini ya Kaze ni mshambuliaji Songne Yacouba ambaye licha ya kocha huyo kumkuta akisotea benchi, amemfanya kiwango chake kuimarika na kuwa tegemeo la timu katika kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho ambapo hadi sasa amefumania nyavu mara mbili na amepiga pasi nne zilizozaa mabao.
Kaze ameendeleza ubora wa wachezaji ambao aliwakuta wakifanya vizuri katika kikosi cha timu hiyo kabla hajapewa jukumu la kuinoa. Kipa Metacha Mnata ameendelea kuwa bora, kiungo Mukoko Tonombe na beki Lamine Moro ambao licha ya ubora wa kiuchezaji hasa katika kuilinda timu, wameendelea kupaa.
Lakini Kaze ambaye mashabiki wanasubiri usajili huo atakaofanya kwenye dirisha dogo, ameibadili timu hiyo kutoka kucheza soka la kujilinda na kuifanya ishambulie.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema; “Kuna mabadiliko makubwa ambayo timu imekuwa ikionyesha chini yake. Inapata matokeo mazuri huku ikicheza vyema ndani ya uwanja tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma.
“Jambo la msingi ni Wanayanga kuendelea kumpa ushirikiano mkubwa kocha huyu na wachezaji kutimiza majukumu yao naamini atatufikisha mbali na atatufanya tutimize malengo yetu.”
Lakini kuhusu matokeo ya sasa Kaze alisema; “Naamini haya ni matunda ya ushirikiano na sapoti kutoka kwa kila mmoja kwenye timu. Ligi ni ngumu na nadhani tunatakiwa kuendelea kujituma zaidi ili tuweze kufanya vizuri.”