Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu afichua siri Simba, kusajili kiungo nyota

Muktasari:

  • Katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Simba itakutana na Stellenbosch.

Wakati Simba ikijihakikishia kiasi cha Dola 750,000 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kufuzu nusu fainali ya kombe la Shirikisho Afrika, kocha mkuu wa timu hiyo Fadlu Davids amefichua mipango ya kumsajili kiungo bora mshambuliaji mzawa ambaye hata hivyo hajamtaja jina.

Ushindi wa mikwaju ya penalti 4-1 dhidi ya Al Masry jana baada ya sare ya mabao 2-2 katika mechi mbili za robo fainali, umeifanya Simba kutinga nusu fainali ambapo itakutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Kwa kuingia nusu fainali, Simba imejihakikishia kiasi cha Dola 750,000 (Sh2 bilioni) ambacho kila timu inayotinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika inakuwa na uhakika wa kuvuna kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Timu inayoishia hatua ya nusu fainali inapata kiasi hicho cha fedha lakini Simba inaweza kupata kitita kikubwa zaidi iwapo itatinga fainali au kuchukua ubingwa wa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa muongozo wa CAF wa mgawanyo wa fedha za zawadi za Kombe la Shirikisho Afrika, timu inayoshika nafasi ya pili katika mashindano hayo inapata kitita cha Dola 1 milioni (Sh2.7 bilioni) na bingwa anapata kiasi cha Dola 2 milioni (Sh5.4 bilioni).

Wakati ikiwa na uhakika wa fedha hizo, kocha Davids amesema kuwa wapo katika mpango wa kumsajili kiungo mshambuliaji mzawa wa daraja la juu ambaye ataiimarisha vilivyo timu yake.

"Tusishekerekee sana kwa sababu bado kuna mambo ya kutimiza zaidi. Huu ni msingi tu, tunaendelea kujiimarisha na tumeshakaa kikao cha usajili ujao tayari na sasa tunamtafuta kiungo namba 10 bora zaidi wa Tanzania na natumaini tutainasa saini yake,” amesema Davids.

Ingawa Davids hajataja jina la kiungo huyo, mchezaji ambaye Simba imekuwa ikiripotiwa inamuwania wa nafasi hiyo ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.

Katika hatua nyingine, Simba imepanda hadi katika nafasi ya nne katika chati ya ubora ya klabu ya CAF kutokana na mjumuisho wa alama ambazo timu zimevuna katika kipindi cha ushiriki wa mashindano ya klabu Afrika kwa kipindi cha miaka mitano ikifikisha pointi 43.

Chati hiyo ndio itatumika katika upangaji wa droo za hatua za awali na makundi katika mashindano ya klabu Afrika msimu ujao wa 2025/2026.

Simba imechukua nafasi ya Zamalek ya Misri yenye pointi 42 ambayo imetupwa nje ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na timu ya Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa ushindi wa bao 1-0.

Nafasi ya kwanza katika chati hiyo inashikiliwa na Al Ahly yenye pointi 78, ikifuatiwa na Mamelodi Sundowns yenye pointi 57 sawa na Esperance na Simba iko nafasi ya nne huku nafasi ya tano ikiwepo RS Berkane yenye pointi 42.

Kuna uwezekano wa Simba kubaki katika nafasi hiyo ya nne au kushuka kutokana na matokeo itakayoyapata katika hatua inayofuata ambapo ikifika fainali au kuchukua Kombe itaongeza pointi na ikiishia nusu fainali maana yake itabakia na pointi 43 ilizonazo.