Kocha Serengeti Boys: Tupeni nafasi muone kazi
Muktasari:
- Kocha huyo aliisaidia Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys kumaliza mshindi wa pili kwenye mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana U-17, yaliyofanyika nchini Morocco Tanzania ikifanikiwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia nchini Qatar.
KOCHA Mkuu wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu, amesema ni wakati sasa kwa wadau wa soka nchini kuendelea kuwaamini makocha wazawa kutokana na uwezo mkubwa wanaouonyesha katika timu za taifa na klabu mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa wao wenyewe kuendelea kupeana moyo na kushirikiana katika safari ya kulijenga soka la Tanzania.
Kocha huyo aliisaidia Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys kumaliza mshindi wa pili kwenye mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana U-17, yaliyofanyika nchini Morocco Tanzania ikifanikiwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia nchini Qatar.
Nsanganzelu amesema mafanikio ambayo yamekuwa yakipatikana katika miaka ya karibuni yanaonyesha wazi kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya makocha wenye uwezo wa kufanya kazi kwa viwango vya juu, kinachohitajika ni kupewa nafasi, muda wa kufanya kazi na mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo amesema wakipeana moyo na kubadilishana uzoefu utasaidia katika maendeleo ya taaluma yao.
“Leo tunaona matokeo ya elimu ambayo makocha wanapata kupitia CAF, FIFA na TFF. Kiwango cha makocha wetu kinazidi kukua kila siku. Kilichobaki ni kuaminiwa zaidi na sisi wenyewe kuendelea kushikamana ili tuweze kufanya vizuri,” amesema.
“Ni wakati wa makocha wazawa kuaminiana na kupeana moyo. Tunapaswa kufurahia mafanikio ya mwenzetu kwa sababu mafanikio yake yanatengeneza njia kwa wengine. Tukisimama pamoja tutafanya makubwa zaidi,” amesema Nsanganzelu.
Hilo linakuja ikiwa siku chache tangu kocha wa Mashujaa FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kuzungumzia kuhusu nafasi ya makocha wazawa kuaminiwa kwenye klabu na timu ya taifa.
“Muda mwingine napenda kujilipua, singoji mpaka nife mje mnisifie, kazi aliyofanya Hemed Suleiman ‘Morocco’, Juma Mgunda na mimi kuipeleka timu ya Taifa AFCON halafu tukatolewa kihuni ni jambo baya sana,” amesema Kihwelo.
Mwaka jana, Morocco aliandika rekodi akiwa kocha wa kwanza mzawa kuiongoza Taifa Stars kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Alifanya hivyo Novemba 2024 baada ya kuiongoza Tanzania kuifunga Guinea bao 1-0 na kukata tiketi ya AFCON 2025.
Mbali na hilo, Morocco aliweka rekodi nyingine ya kuwa kocha wa kwanza Mtanzania kuwa sehemu ya benchi la Taifa Stars katika AFCON mara tatu mfululizo. Mwaka 2019 alikuwa kocha msaidizi chini ya Emmanuel Amunike, mwaka 2023 akiwa msaidizi wa Adel Amrouche na mwaka 2025 akiwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Katika CHAN 2024, Morocco aliipeleka Tanzania robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo.