Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Stellenbosch: Simba ni timu hatari CAF

Muktasari:

  • Jumapili hii, Simba itakuwa mwenyeji wa Stellenbosch katika nusu fainali ya mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kocha wa Stellenbosch FC, Steve Barker, amesema Simba SC ni moja ya timu hatari zaidi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, akisisitiza kuwa ubora wa Wekundu wa Msimbazi hauishii kwa kikosi cha kwanza pekee, bali unakwenda hadi wachezaji wa akiba.

Jumapili hii, Simba itakuwa mwenyeji wa Stellenbosch katika nusu fainali ya mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kabla ya mchezo huo, Barker amesema wamefanya uchambuzi wa kina kuhusu wapinzani wao kupitia msaada wa makocha wake wasaidizi raia wa Afrika Kusini ambao ni marafiki wa karibu na benchi la ufundi la Simba.

“Ndiyo, tumefanya uchambuzi wetu. Kocha Fadlu (Davids) na Kocha Darian (Wilken) ni marafiki wa karibu na makocha wetu wasaidizi, kwa hiyo tumekuwa tukifuatilia mwenendo wa Simba na maendeleo yao,” amesema Barker.

Kocha huyo amesema Simba wameonyesha uthabiti wa kiwango cha juu kwa miaka mingi kwenye mashindano ya CAF, jambo linalothibitisha ubora wa kikosi hicho.

“Simba wana wachezaji wazuri mno kwenye ushambuliaji, wana nguvu kubwa katika maeneo ya pembeni, wachezaji wenye uwezo wa kutembea na mpira, kufunga na kutengeneza nafasi. Pia wana safu imara ya ulinzi. Kwa kweli ni timu kamili,” amesema.

Barker amesema licha ya kutambua wapo wachezaji wawili au watatu muhimu zaidi kwa Simba, haitakuwa busara kuwaangalia wao pekee kama tishio.

“Itakuwa ni kosa kufikiria kwamba Simba wana hatari kwa wachezaji wachache tu. Hii ni timu hatari kuanzia kwa kipa hadi kwa wachezaji wa akiba. Hata benchi linaweza kuleta mabadiliko ya kweli,” ameongeza.