Malindi, Mafunzo zaifuata KMKM fainali

Muktasari:
- Malindi iliichapa Black Sailors kwa penalti 4-1, ilihali Mafunzo waliwanyoosha maafande wenzao wa Kundemba pia kwa penalti 2-0 mechi hizo zikipigwa viwanja vya Mao.
TIMU za Malindi na Mafunzo jioni ya leo Alhamisi zimetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Zanzibar (ZFF Cup) Kanda ya Unguja, baada ya kupata ushindi katika mechi za robo fainali dhidi ya Black Sailors na Kundemba.
Malindi iliichapa Black Sailors kwa penalti 4-1, ilihali Mafunzo waliwanyoosha maafande wenzao wa Kundemba pia kwa penalti 2-0 mechi hizo zikipigwa viwanja vya Mao.
Katika mechi kati ya Malindi na Black Sailors, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilishuhudiwa timu hizo zikifungana bao 1-1.
Malindi ilitangulia kwa bao la dakika ya nane lililowekwa kimiani na Ali Miraji kabla ya Suleiman Khamis kulichomoa dakika ya 32.
Kipindi cha pili timu zote ziliongeza kasi ya mashambulizi kusaka mabao ya ziada, lakini haikusaidia kitu kwani dakika 90 ziliisha matokeo yakiwa ni sare ya 1-1, ndipo ikaamuliwa kupigiana penalti na Malindi kushinda 4-1 na kufuzu nusu fainali kuzifuata KMKM na Mlandege zilizotangulia mapema jana.
Mara baada ya mechi kumalizika, Kocha wa Malindi, Suleiman Mohamed 'Kocha Mo', amesema hiyo ni mechi ya pili kushinda kwa matuta, hivyo anaendelea kuwaandaa wachezaji ili wafanye vizuri mechi zijazo.
Kocha Mo, amesema amegundua timu hiyo, ina tatizo kubwa la kupoteza umakini ikiwa uwanjani kwani wanashambulia na kutengeneza nafasi ila wanashindwa kumalizia kwa kufunga.
"Tunatengeneza nafasi nyingi, lakini hatumbukizi mipira wavuni, kama tungekuwa makini tungemaliza mechi ndani ya dakika 90 tu," amesema Kocha Mo, huku kocha wa Black Sailors, Khamis Ali Khamis 'Morinyo' akisema timu hiyo imejitahidi kufanya vizuri dakika 90, ila penalti ndizo zimetoa mshindi na siki zote mikwaju hiyo haina mwenyewe.
Amesema wanarudi mazoezini kujinoa vizuri kwa lengo la kuipambania mechi zilizosalia za ligi wanayoshiriki.
Katika mechi nyingine ya robo fainali, Mafunzo iliibuka ushindi wa penalti 2-0 dhidi ya Kundemba, baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
Katika kupigiana mikwaju hiyo ya penalti, Mafunzo ikaibuka kidedea kwa kutumbikiza 2-0 na kufuzu nusu fainali ikiungana na KMKM, Malindi na Mlandege kusaka mshindi wa Kanda ya Unguja ambayo msimu uliopita ilikuwa ni JKU iliyoenda kupoteza mezani mbele ya Chipukizi iliyoibuka Bingwa, jambo haikwenda kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Nafasi yake ilichukuliwa na Uhamiaji iliyotolewa mapema na Al Ahli Tripoli ya Libya ambayo nayo iling'olewa na Sba raundi ya pili kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1.
Simba kwa sasa ipo fainali ikijiandaa kuvaana na wanafainali wa msimu uliopita, RS Berkane ya Morocco ambayo ilipoteza mbele ya Zamalek ya Misri ambayo msimu huu ililitema taji katika hatua ya robo fainali mbele ya Stellenbosch ya Afrika Kusini iliyolewa na wawakilishi hao wa Tanzania wikiendi iliyopita.