Mashabiki Simba wataka mechi iishie Zanzibar

Muktasari:
- Moses maarufu kama Pasi Milioni, ambaye ametoka jijini Dar es Salaam amesema kuwa Simba imeiva na ina kikosi kipana chenye uzoefu wa mechi kubwa, hivyo hana shaka na matokeo.
Mashabiki wa Simba ambao wamesafiri kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania wanaamini kuwa timu yao itaimaliza vizuri mechi ya nusu fainali kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, na safari ya Afrika Kusini itakuwa ni kwa ajili ya kufanya shopingi.
Moses maarufu kama Pasi Milioni, ambaye ametoka jijini Dar es Salaam amesema kuwa Simba imeiva na ina kikosi kipana chenye uzoefu wa mechi kubwa, hivyo hana shaka na matokeo.
"Hii mechi tunaiua hapa hapa Amaan. Safari ya Afrika Kusini wikeindi ijayo ni kama kwenda kutalii tu. Mimi mwenyewe naenda huko, si kwa presha ya mechi bali kwa ajili ya kununua viatu, nguo na perfumes," amesema Pasi Milioni.
Ameongeza kuwa, tofauti na misimu iliyopita, safari ya Simba hadi hatua ya nusu fainali msimu huu imejengwa kwenye umoja wa timu na benchi la ufundi thabiti jambo linalowapa mashabiki matumaini makubwa.
Rehema Nassor, shabiki kutoka Morogoro, amesema kuwa pamoja na heshima kwa Stellenbosch, haoni kama wana uwezo wa kuisimamisha Simba.
"Tunajua mechi ni dakika 90, lakini naamini Simba watakuwa na uamuzi mzito Amaan. Watanzania tunahitaji fainali. Na sisi akina mama tumejiandaa hata na mashati ya 'final bound'," amesema Rehema.
Kwa upande wake, Hamisi Komba kutoka Mtwara amesema kuwa hata kabla ya mechi, alishakata tiketi ya kwenda Cape Town kwa ajili ya kutazama marudio, ila zaidi kwa sababu ya matembezi na kufanya manunuzi.
"Simba si ya mchezo, Amaan lazima itang’ara. Mie nilisema, nikiwa Afrika Kusini niende Mall of Africa tu. Mechi ni bonus," amesema huku akicheka.
Mashabiki hao walisema hali ya Zanzibar kuwa mwenyeji wa mechi hiyo imeongeza ladha ya soka, huku wengine wakieleza kuwa ni mara yao ya kwanza kufika visiwani humo na wamefurahia mapokezi ya Wazanzibari.
Mchezo huo wa nusu fainali ya kwanza umeelezwa kuwa wa kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa visiwa hivyo kuwa mwenyeji wa hatua hiyo kwenye michuano ya CAF, jambo linalowafanya mashabiki wa Simba kuhisi kuwa ni ishara ya mafanikio.
Mashabiki wengi wa Simba walionekana kuvaa jezi za timu yao, wengine wakiwa na vuvuzela, skafu na mabango yenye ujumbe wa hamasa kwa wachezaji wao wakiongozwa na kocha Fadlu Davids.