Mido Biashara United akiri mambo magumu

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Wagana aliyewahi kuichezea pia Mbuni FC ya jijini Arusha, alisema kitendo cha kukatwa pointi 15, huku aliyekuwa rais na mfadhili wa kikosi hicho, Revocatus Rugumila kuondoka kimechangia hali ngumu ya kiuendeshaji.
KIUNGO mshambuliaji wa Biashara United, Pascas Wagana amesema wana kazi kubwa ya kukipambania kikosi hicho kubakia Ligi ya Championship, baada ya malengo ya awali ya kuirejesha Ligi Kuu Bara kuota mbawa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Wagana aliyewahi kuichezea pia Mbuni FC ya jijini Arusha, alisema kitendo cha kukatwa pointi 15, huku aliyekuwa rais na mfadhili wa kikosi hicho, Revocatus Rugumila kuondoka kimechangia hali ngumu ya kiuendeshaji.
"Bado hatujakata tamaa kwa sababu gepu la pointi na waliokuwa juu yetu sio kubwa, tunachopambana ni kuibakisha timu kwa msimu ujao na wala sio vinginevyo, ikitokea tumepata nafasi hata ya kucheza tu 'Play-Off', kwetu itakuwa ni mafanikio."
Kauli ya nyota huyo inajiri baada ya timu hiyo kupokwa pointi 15, kutokana na kuandamwa na ukata ulioifanya kushindwa kusafiri kwenda Mbeya kucheza dhidi ya Mbeya City uliotakiwa kuchezwa Desemba 3, mwaka jana.
Kitendo cha kupokwa pointi 15, kimeifanya timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2021-2022, kupambana kwa ajili ya kubakia msimu ujao, kwani licha ya kushinda michezo mitano, sare minne na kupoteza 13, ila inaburuza mkiani na pointi zake nne.