Prime
Mukwala aishtukia Dabi, apiga mkwara

Muktasari:
- Mukwala ambaye alifunga mabao hayo na kuifanya Simba kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Yanga kutoka saba hadi nne huku wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja, ameonyesha kuwa tayari kwa Kariakoo Dabi wikiendi ijayo.
MSHAMBULIAJI wa Simba, Steven Mukwala mfungaji wa mabao matatu (hat-trick) katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, anaamini mchezo ujao dhidi ya Yanga utakuwa mgumu zaidi ya ilivyokuwa dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Mukwala ambaye alifunga mabao hayo na kuifanya Simba kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Yanga kutoka saba hadi nne huku wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja, ameonyesha kuwa tayari kwa Kariakoo Dabi wikiendi ijayo.
"Mechi dhidi ya Yanga itakuwa tofauti kabisa na ile ya Coastal Union. Hawa ni wapinzani, wana nguvu na mbinu nzuri. Tumejua vema Yanga wanajua kubadilika na kucheza kwa umakini mkubwa. Kwa hiyo, si mchezo wa rahisi," alisema mshambuliaji huyo kutoka Uganda.
Mkwala mwenye mabao manane kwenye ligi, anaonyesha kuwa kila mechi ina changamoto zake, hivyo, lazima Simba iwe imara zaidi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri wikiendi ijayo.
Katika mchezo wao dhidi ya Coastal Union, Mukwala alionyesha uwezo mkubwa kwa kufunga mabao matatu yaliyoisaidia Simba kuondoka na ushindi wa 3-0. Alisema ushindi huo ulikuwa muhimu sana kwa timu, kwani uliongeza morali na kuwatia nguvu wachezaji katika mchezo wa derby dhidi ya Yanga Machi 8.
"Ushindi huu dhidi ya Coastal ulikuwa wa muhimu sana kwetu. Tumepata pointi tatu, pia tumetengeneza morali kubwa kwa ajili ya mechi kubwa inayokuja," alisisitiza.
Mukwala alieleza, licha ya kutopata nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo katika michezo mingi msimu huu, yupo tayari kutumika wakati wowote atakapohitajika.
"Kwa kweli, mimi sina tatizo na hilo. Kocha (Fadlu Davids) anajua ni lini ananihitaji na mimi nitakuwa tayari kila wakati. Kama ilivyokuwa dhidi ya Coastal, nilikuwa tayari kutumikia timu na kushirikiana na wachezaji wenzangu," alisema Mukwala.
Aliongeza, yeye ni mchezaji wa timu na anachofanya ni kuhakikisha anatoa mchango wake kwa timu kila inapohitajika. "Hakuna shaka, nafasi ya kucheza au kutocheza inategemea mbinu za kocha. Mimi ni sehemu ya timu na kila wakati najitahidi kutoa kilicho bora kwa timu yangu," alisema.
MUKWALA AU ATEBA
Miongoni mwa vitu ambavyo kocha wa Simba, Fadlu Davids amekuwa akivifanyia kazi ni changamoto kwenye safu yake ya ushambuliaji, licha ya kuonekana kumtumia zaidi Lionel Ateba mwenye mabao manane huku manne yakiwa ya mikwaju ya penalti, pia ameonyesha kuwa na imani na Mukwala.
Mfano mzuri kabla ya mchezo dhidi ya Coastal Union, alimpa dakika zaidi ya 60, Mukwala katika mechi za mazoezi ambayo ilifanyika katika uwanja wa Mo Simba Arena, alihitaji mchezaji huyo pamoja na wengine ambao hawakuwa na nafasi katika michezo iliyopita kuwa tayari wakihitajika.
Mukwala alionekana kufanya vizuri na inawezekana ndio sababu iliyochochea Fadlu kuamua kumpa nafasi dhidi ya Coastal na kwa kiwango alichokionyesha mshambuliaji huyo ni wazi Fadlu atakuwa na mtihani wa kufanya maamuzi ya nani wa kuanza naye wikiendi ijayo dhidi ya Yanga.
MSIKIE PLUIJM
Kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm ambaye anamfahamu vizuri Mukwala tangu akiwa Asante Kotoko ya Ghana, ana imani kubwa na uwezo wa mshambuliaji huyo. Pluijm, ambaye kwa sasa anaishi Ghana pamoja na familia yake, alisema Mukwala ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anahitaji tu kupata fursa zaidi ili kuwa tishio.
"Mukwala ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Nilimfahamu vizuri akiwa Asante Kotoko na kama atapata fursa ya kucheza mara kwa mara, atakuwa mchezaji hatari zaidi," alisema Pluijm.
Pluijm aliongeza kadiri muda unavyosogea, ndivyo Mukwala anavyokuwa katika kiwango bora zaidi. "Mukwala anaendelea kuwa bora kila anapocheza. Ana kasi, ana akili ya mchezo, na ni mchezaji ambaye anajua jinsi ya kufunga. Ikiwa atapata nafasi ya kucheza kwa mara nyingi, anaweza kuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kwenye ligi," alisema.