Prime
Mwalimu 'ampima mguu' Dube, amvizia na rula ya dhahabu
MSHAMBULIAJI wa Simba, Seleman Mwalimu amemtumia salamu mwenzake wa Yanga, Prince Dube akimwambia anakitaka kiatu cha dhahabu ambayo ni tuzo maalum kwa mfungaji bora wa mashindano.
Mwalimu na Dube wana jambo lao msimu huu ambapo kule kwenye Ligi Kuu Bara, Dube anaongoza kwa kufunga mabao nane sawa na Fabrice Ngoy wa Namungo, huku Mwalimu akifunga sita akiwa kinara ndani ya Simba.
Pia Dube anaongoza kwa ufungaji kwenye Kombe la Muungano akiwa na mabao matatu, akifuatiwa na Mwalimu aliyefunga mawili na wote wawili watashuka dimbani Jumatano hii kuzipambania Yanga na Simba kwenye mchezo wa fainali wa michuano hiyo utakaothibitisha nani atamaliza kinara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalimu amesema anaitaka tuzo ya ufungaji bora akianzia kwenye mashindano ya Muungano na kwa namna Simba inavyocheza anaamini ataweza kufanya kweli.
Mwalimu amesema ubora wa timu hiyo ndio umempa wepesi wa kuzidisha kasi ya kufunga akifurahia kucheza na viungo wabunifu ambao wamekuwa wakimtengenezea pasi nyingi. “Kweli naitaka tuzo ya ufungaji bora, kila mshambuliaji ana ndoto hiyo ya kuwa mfungaji bora na mimi nitaanzia hapa kwenye Muungano, najua kuna mtu yupo juu yangu lakini nitapambana kutafuta mabao kwenye mchezo wa fainali,” amesema Mwalimu.
“Kitu ninachofurahia ni kucheza kwenye timu yenye viungo wengi wabunifu, kila mshambuliaji angependa kucheza kwenye kikosi cha namna hii, nimekuwa nafunga ni kutokana na ubora wa viungo wa timu yetu.”
Aidha Mwalimu ameongeza katika kiu yake hiyo anatamani itimie ili aweze kuwabeba kwa heshima wachezaji wazawa katika kuichukua tuzo hiyo kutokana na wageni wengi kutawala eneo hilo.
“Ninapoipigania tuzo hii nawafikiria pia wachezaji wenzangu wazawa, unajua wenzetu wa kigeni wamekuwa wanachukua sana mafanikio haya lakini kwangu nataka iwe zamu ya sisi wazawa pia.”