Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu kutesti na Sevilla, Porto

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa tovuti ya Wydad, timu hiyo itacheza mechi mbili za kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia inayotarajiwa kuanza Juni 15, 2025 hadi Julai 13, 2025 nchini Marekani.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Wydad Casablanca ya Morocco, Selemani Mwalimu Abdallah ‘Gomez’ anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mechi mbili dhidi ya Sevilla ya Hispania na Porto kutoka Ureno.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wydad, timu hiyo itacheza mechi mbili za kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia inayotarajiwa kuanza Juni 15, 2025 hadi Julai 13, 2025 nchini Marekani.

"Mechi hizi mbili ni sehemu ya programu ya maandalizi yetu yanayolenga kupima utayari wa timu na kuimarisha viwango vya wachezaji kabla ya kuanza mashindano," imeeleza taarifa ya Wydad.

Wakati Wydad ikitoa taarifa hiyo, Sevilla imethibitisha kwa kusema mechi dhidi Wydad itachezwa Mei 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mohammed V uliopo Casablanca nchini Morocco, huku ile ya Porto ikiwa bado haijawekwa wazi.

"Kikosi chetu cha kwanza kitacheza mechi ya kirafiki nchini Morocco dhidi ya Wydad Athletic Club siku ya Jumanne, Mei 27. Mechi hiyo itaanza saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca," imesema taarifa ya klabu hiyo.

"Katika mechi hii, tutapambana dhidi ya moja ya timu zilizofanikiwa sio tu nchini Morocco bali Afrika nzima. Wydad AC ni moja ya timu mwakilishi wa Afrika katika Klabu Bingwa ya Dunia baada ya kushinda Ligi ya Mabingwa Afrika 2022. Kupitia ratiba hii, tutapanua wigo wetu nchini Morocco, mojawapo ya nchi ambapo mashabiki wetu wanaongezeka na kukua."

Wydad ni kati ya timu 32 zitakazoshiriki michuano hiyo huku wawakilishi wengine wa Afrika ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance (Tunisia) na Al Ahly (Misri)

Katika michuano hiyo, Wydad imepangwa Kundi G na timu za Manchester City ya England, Al Ain (United Arab Emirates) na Juventus (Italia).

Mechi ya kwanza Wydad itacheza Juni 18 dhidi ya Manchester City, kisha Juni 22 dhidi ya Juventus na kumaliza hatua ya makundi Juni 26 ikipambana na Al Ain.

Akizungumzia michuano hiyo, Gomez aliyejiunga na Wydad Januari 31, 2025 akitokea Singida Black Stars kwa mkataba hadi Juni 30, 2029, amesema: “Unajua kupata tu nafasi ya kujiunga na timu hii kwangu ni fursa kubwa. Pia kitendo cha hii timu kupata nafasi ya uwakilishi kwenye michuano hiyo na jina langu likiwa miongoni mwa nyota wa kikosi cha Wydad ni mafanikio makubwa.

“Nafurahia maisha ndani ya nchi hii, changamoto ya kukosa namba inaniongeza nguvu ya kupambana. Nashukuru nimekuwa nikipata walau dakika chache za kucheza, hizo ninazozipata zinanipa nguvu ya kuonyesha kitu ili kulishawishi benchi liendelee kuniamini.”

Tangu ajiunge na Wydad, Gomez amecheza mechi tatu za Ligi Kuu Morocco akitumika kwa dakika 36. Mechi ya kwanza dhidi ya COD Meknes alicheza kwa dakika 30 iliyomalizika kwa matokeo ya 0-0, kisha dhidi ya Ittihad Tanger iliyomalizika kwa sare ya 1-1 akitumika kwa dakika tano na dhidi ya JS Soualem wakati Wydad ikishinda 2-0, alicheza kwa dakika moja.