Ni Sowah tena Singida BS ikiikaanga Fountain Gate

Muktasari:
- Katika mchezo huo wa ligi kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Singida Black Stars licha ya kuwa ugenini ilitawala muda mwingi na kuwafanya msimu huu kukusanya pointi zote sita dhidi ya Fountain Gate ikiifunga mabao matano baada ya mzunguko wa kwanza kushinda 2-0 na leo ikishinda 3-0.
ACHANA na ushindi wa mabao 3-0 walioupata Singida Black Stars, ishu ni mshambuliaji wa timu hiyo, Jonathan Sowah ambaye ametupia bao lake la nane msimu huu.
Katika mchezo huo wa ligi kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Singida Black Stars licha ya kuwa ugenini ilitawala muda mwingi na kuwafanya msimu huu kukusanya pointi zote sita dhidi ya Fountain Gate ikiifunga mabao matano baada ya mzunguko wa kwanza kushinda 2-0 na leo ikishinda 3-0.
Sowah ndiye aliyeanza kuwanyanyua mashabiki wachache waliojitokeza kwenye uwanja huo katika dakika ya 30 ikiwa ni bao lake la nane kwenye mechi nane alizocheza tangu ajiunge na timu hiyo dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, 2025.
Bao la Sowah lilidumu hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza na kuitoa timu hiyo kifua mbele.
Kipindi cha pili wageni wa mchezo huo waliendelea kuliandama lango la wapinzani na kufanikiwa kuandika bao la pili dakika 56 kupitia Frank Assink na bao la tatu likiwekwa kimyani na Emmanuel Keyekeh dakika ya 71 kwa faulo ya moja kwa moja.
Ushindi huo wa mabao 3-0 unaifanya Singida Black Stars kuendelea kusalia nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 47 baada ya mechi 24 na kuikaribia Azam FC yenye pointi 48 ikiwa na michezo 23 ikitarajiwa kushuka dimbani kesho Alhamisi dhidi ya KenGold ugenini.
Fountain Gate baada ya kupoteza mchezo huo imebaki nafasi ya saba na pointi 27 kwenye mechi 24 walizocheza wakishinda nane, sare nne na vipigo 12, wamefunga mabao 28 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 23.