Pacome apata jeuri ya ubingwa

Muktasari:
- Kiungo fundi huyo ambaye kwa upande wa Yanga anaongoza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo msimu huu akichukua mara tano, alisema wanatambua ubora wa wapinzani walio mbele yao kwenye michezo saba iliyobaki lakini hawana hofu kutokana na ubora na malengo waliyojipangia kuhakikisha wanatetea taji la ligi.
KIWANGO bora kinachoendelea kuonyeshwa na Yanga huku ikipata ushindi mfululizo ugenini na nyumbani, imempa jeuri kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Yanga, Pacome Zouzoua ambaye ameliambia Mwanaspoti kuwa hawaoni timu ya kuwazuia kutetea taji la Ligi Kuu Bara msimu huu.
Pacome ambaye amehusika kwenye mabao 15 msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara akifunga saba na kutoa asisti nane, amesema ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Tabora United umedhihirisha kwa sasa hawana utani na malengo yao ya kutetea ubingwa.
“Yanga ni ile ile ya msimu uliopita, kitu kikubwa kilichobadilika ni kwa wachezaji pekee ambao kila mmoja anaonyesha kujipambania na kuipambania timu, hivyo ukiunganisha unapata timu bora na ya ushindani.
“Hicho ndicho kinachofanyika sasa na naamini kwenye mechi zilizobaki tukichanga vizuri karata zetu tutaendelea tulipoishia.
“Kila mechi iliyo mbele yetu tunaichukulia kama fainali, tunawaheshimu wapinzani wetu wote, hakuna timu changa wala kongwe kwenye ligi, tunaamini katika ushindani. Malengo yetu kwa sasa ni kukusanya pointi kwenye kila mchezo hivyo imani kubwa ni maandalizi bora bila kujali tunakutana na timu ya aina gani,” amesema Pacome.
Kiungo fundi huyo ambaye kwa upande wa Yanga anaongoza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo msimu huu akichukua mara tano, alisema wanatambua ubora wa wapinzani walio mbele yao kwenye michezo saba iliyobaki lakini hawana hofu kutokana na ubora na malengo waliyojipangia kuhakikisha wanatetea taji la ligi.
Akizungumzia ubora wake kwa ujumla, raia huyo wa Ivory Coast alisema unachangiwa na morali nzuri ya kikosi cha timu hiyo ambacho ameweka wazi kuwa wanacheza kwa kushirikiana na kuipambania timu ambayo ina malengo makubwa kuhakikisha inakuwa bora ndani na kimataifa.
“Ushirikiano mzuri ninaoupata kutoka kwa wenzangu na pia kuaminiwa na benchi la ufundi licha ya ushindani mkubwa wa namba kwenye eneo ninalocheza, ndio kitu kinanifanya nipambane na kumuonyesha kocha kuwa hajakosea kunipa nafasi kwa kufanya majukumu yangu kwa ubora,” amesema.
Pacome alijiunga na Yanga msimu wa 2023/24 akitokea Ligi Kuu ya Ivory Coast alikokuwa mchezaji bora wa msimu (MVP) na alikuja kuongeza nguvu katika eneo la kiungo mshambuliaji akisaidiana na Stephane Aziz Ki, kinara wa upachikaji mabao msimu huo akifunga 21.
Nyota huyo msimu wake wa kwanza Yanga alipachika mabao saba na asisti nne katika mechi 23 akitumika kwa dakika 1520. Kwa idadi hiyo ya msimu wa kwanza, Pacome alihusika katika mabao 11 kati ya 71 yaliyofungwa na timu hiyo ikitwaa ubingwa wa tatu kwa kukusanya pointi 80 katika mechi 30.
Hivi sasa Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 61 baada ya kucheza mechi 23, ikishinda 21, sare 1 na kupoteza 2, huku ikifunga mabao 61 na kuruhusu tisa.