Saido afunguka, awataja Simba

Muktasari:

STAA wa Yanga aliyeleta presha kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa sasa, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ amevunja ukimya na kufunguka kila kitu juu ya sakata lake Jangwani, huku akiwataja Simba.

STAA wa Yanga aliyeleta presha kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa sasa, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ amevunja ukimya na kufunguka kila kitu juu ya sakata lake Jangwani, huku akiwataja Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Saido alisema haoni kama wanaomuandama mitandaoni ni mashabiki wa Yanga na kwamba anahisi wanaofanya hivyo kwa lengo la kumvuruga ni watani wao Simba.

Mshambuliaji huyo, alisema anajua mashabiki wa Simba ndio wanaozidisha vurugu kwake mitandaoni na kwamba wala hilo halimsumbui na anaielekeza akili yake kuhakikisha Yanga inafanikiwa uwanjani.

“Nasikia kelele nyingi huko mitandaoni binafsi, mimi huwa sifuatilii sana hizo taarifa za huko, hivyo sidhani kama wanaoeneza vurugu hizo eti ni shabiki wa Yanga nadhani hawa watakuwa watu wa Simba,” alisema Saido na kuongeza;

“Ninachoshangaa kama kuna watu wa Yanga nao watakuwa wameingia katika mtego huo, mimi niko sawa na naielekeza akili yangu katika maandalizi ya mechi za timu yangu.”

Akizungumzia tukio la kudaiwa kufuta picha zake za Yanga katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, Saido alisema tangu amefika nchini hajawahi kuweka taarifa yoyote katika akaunti yake hiyo.

“Unajua wapo ambao tangu nimefika hapa wamekuwa wakifungua akaunti mbalimbali za jina langu, mimi nina akaunti moja tu ya Instagram ambayo inatiki ya bluu ina jina la Ntibazonkiza.

“Hii akaunti sijaitumia muda mrefu kwa kuwa ilikuwa ina shida na niliposaini Yanga tu niliwaomba watu wa tehama (IT) wanisaidie kuifanyia kazi na mpaka sasa bado halijakamilika,” alisema Saido na kuongeza; “Akaunti hiyo sijaweka posti yoyote ile kwa kuwa siwezi kufanya hivyo kutokana tatizo lililotokana na wao Instagram, sasa nashangaa wanaosema nimefuta picha, sijui waliona nimeweka picha gani, kama yupo ambaye ana uhakika nimefuta picha aje nayo anionyeshe.”

Mkali huyo mwenye mabao matatu na asisti nne mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara, alisisitiza; “ Hizo akaunti nyingine naziangalia tu watu wanaokota picha wanaziweka wanaandika vitu vyao nigewasihi watu wasimuamini mtu huko kwa sasa sina akaunti ninayoitumia, akaunti yangu ikikaa sawa nitatoa taarifa.”

Akizungumzia sakata lake la kutaka kutoka uwanjani katika mchezo dhidi ya Gwambina mara tu baada ya kufunga bao, Saido alisema hilo lilishapita na kila binadamu ana uwezo wake wa kudhibiti hasira zake.

“Napenda kuisaidia timu yangu natamani kuona Yanga inashinda mechi zake kwa urahisi, shauku hiyo ndio iliyosababisha yale kutokea. Kila binadamu ana kiwango chake cha kuhimili hasira, nina moyo. wakati ule moyo wangu uliona ufanye kile.

“Kwasasa hayo yameisha nafurahi kuona maisha yamerudi katika utulivu, sote tunashirikiana,” alisema.