Simba mpya hii hapa, mastaa wapya wafichwa Dar

Muktasari:

  • Simba imevutiwa zaidi na uwezo wa winga huyo ambaye msimu uliopita alicheza mechi 30 na kufunga mabao matano na asisti tatu huku msimu mmoja nyuma akifunga mabao manne na kutoa asisti sita katika mechi 30 alizoichezea

MWANASPOTI linajua Simba imekamilisha usajili wa winga matata Joshua Mutale (22) kutoka Power Dynamos ya Zambia kwa mkataba wa miaka mitatu na tayari imemshusha nchini, huku ikimficha kwenye moja ya hoteli za kifahari jijini Dar es Salaam.

Unavyosoma hapa, vigogo wa usajili wa Simba chini ya Cresentius Magori wamemshusha pia kiungo, Debora Fernandes Mavumbo kutoka Mutondo Stars ya Zambia wote wakisubiri kipyenga cha kuanza kwa kambi ya kujiandaa na msimu mpya ambayo ni Ismailia Misri kuanzia Jumatatu.

Mwanaspoti linajua Mutale amesaini tayari miaka miwili  kuitumikia Simba baada ya kufikia muafaka tangu akiwa kwao Zambia.

Simba imevutiwa zaidi na uwezo wa winga huyo ambaye msimu uliopita alicheza mechi 30 na kufunga mabao matano na asisti tatu huku msimu mmoja nyuma akifunga mabao manne na kutoa asisti sita katika mechi 30 alizoichezea Dynamos kwenye Ligi Kuu Zambia.

Mutale aliyeivutia Simba kwa umri mdogo, alitua nchini tangu Jumatatu ya wiki hii kwa ndege ya Air Tanzania.

Moja kwa moja alipelekwa hoteli kwa mapumziko na Jumanne alipelekwa Hospitali ya Muhimbili kufanyiwa vipimo kisha akapelekwa klabuni kupiga picha na video za utambulisho ambao utatangazwa muda wowote kuanzia sasa.

Katika mitandao ya kijamii, Mutale alionekana akiwa uwanja wa ndege  wa Simon Mwansa Kapwepwe International, akiwa na mkewe na mtoto wao ambao walimsindikiza.

Mwanaspoti linafahamu pamoja na Mutale anaiandalia familia yake mazingira sahihi ya kuja kuishi jijini Dar es Salaam na uongozi wa Simba unaendelea kumtafutia nyumba kali.


SIMBA MPYA IMEANZA KUONEKANA

Kabla ya Jumatatu asubuhi Simba yote itakuwa imejulikana. Siku hiyo mapema kabisa itapaa kwenda kambini’Pre Season’ nchini Misri.

Hadi sasa imekamilisha usajili wa wachezaji wasiopungua watatu, pia imeendelea kuwapa ‘Thank You’ baadhi ya nyota waliokuwepo kikosini hapo msimu uliopita na kuwaongezea mikataba mastaa wengine.

Pia Simba ilimtambulisha beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union na ipo mbioni kumtambulisha kiungo Omary Abdallah Omary kutoka Mashujaa.

Hapo wanafika wachezaji wanne wapya ambao mambo yasipobadilika msimu ujao watakipiga Msimbazi na watano ni mshambuliaji Steven Mukwala kutoka Uganda ambaye msimu uliopita alikuwa akikipiga Asante Kotoko na muda wowote kuanzia sasa atatua nchini kusaini mkataba kwani makubaliano ya kila kitu yamefikiwa kwa njia ya simu.

Mwanaspoti linajua Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah Mhena ‘Try Again’, yuko DR Congo na inaelezwa ameenda kukamilisha dili za wachezaji watatu.

Ni beki wa kati, Idumba Fasika aliyewahi kukipiga Valerenga ya Norway, Cap Town City ya Afrika Kusini na FC Saint Eloi ya DR Congo. Mwingine ni Winga Elie Mpanzu kutoka AS Vita.

Haijaishia hapo, Simba pia ipo kwenye mazungumzo mazuri na kiungo mkabaji Agustine Okejepha kutoka Rivers United na huenda wakafikia muafaka wa kusaini mkataba.

Okejepha anatajwa kama mrithi sahihi wa Sadio Kanoute aliyemaliza Mkataba Msimbazi sambamba na Babacar Sarr anayetajwa kuvunjiwa mkataba ingawa bado pande zote mbili hazijafika muafaka.

Tayari Simba imeachana na Shaban Chilunda, John Bocco, Saidi Ntibanzokiza, Henock Inonga, Luis Miquissone na Kennedy Juma huku wengine wengi wakitarajiwa kuagwa siku chache zijazo.