Simba SC yaisogelea Yanga juu

Simba imeendeleza moto wa kula viporo vyake baada ya jana kuwachapa wenyeji wao Mbeya City kwa bao 1-0, shukrani kwa kazi ya kiume ya mshambuliaji John Bocco aliyeitoa kibabe timu yake.
Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Simba kupata ushindi huo baada ya wenyeji kuonyesha tofauti kubwa wakicheza soka la pasi na kasi lakini shida yao ikaja katika kumalizia wakikutana na ukuta mgumu wa wekundu hao chini ya mkongwe Joash Onyango na Ibrahim Ame ambaye jana alipata nafasi nyingine ya kuanza katika kikosi cha kwanza.
Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi kali dakika ya 20 na krosi ya Clatous Chama almanusura iitangulize timu yake, Bocco akishindwa kuunganisha na mpira kugonga mwamba na kipa Lameck Kanyonga kuuwahi.
Muda mrefu wa mchezo huo timu zote zilionekana kushindana kwa soka la katikati ya kiwanja wakishindwa kufika vyema katika kumalizia kufunga.

Ukuta wa Simba ulilazimika kufanya kazi ya ziada kupambana na mshambuliaji mwenye wa na Onyango.
Bocco dakika ya 33 akabadili ubao wa mabao akifunga bao safi la ufundi akipokea mpira kwa mguu wa kushoto kisha kumtoka kwa akili beki Juma Shemvuni na kufunga kwa shuti la ufundi akitumia mguu wa kulia akipokea pasi ya Chama.
Bao hilo lilikuwa ni la nane kwa msimu huu kwa Bocco akiendelea kufufua matumaini ya kuchukua tena kiatu cha ufungaji bora msimu huu huku bao hilo pia likiwa la 32 kwa timu yake.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha wenyeji na kuanza kujipanga tena kwa utulivu ambapo dakika 35 Seleman Ibrahim almanusura afunge bao kwa kichwa akipokea krosi kali ya Mpoki Mwakinyuke iliyowapita mabeki wa Simba na kukutana nayo nyuma yao.
Simba waliendelea kuliandama lango la Mbeya City ambapo dakika ya 37, Keneth Kunambi alifanya kazi nzuri kumbana Bocco aliyekuwa anasubiri kupiga bao la pili akiokoa krosi nzuri ya beki wa kulia Shomari Kapombe.
Simba ilipata nafasi nzuri katika kumaliza dakika 45 za kwanza lakini Meddie Kagere alishindwa kumalizia kwa kishwa krosi ya Hassan Dilunga.
Bao hilo lilidumu hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika kwa Simba kutoka kifua mbele dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine Mkoani Mbeya.
Kipindi cha pili Simba waliingia kwa mabadiliko wakimtoa Bocco nafasi yake ikichukuliwa Chriss Mugalu akirejea baada ya kukaa nje kwa muda mrefu akiwa majeruhi.
Licha ya kuwa na mabadiliko hayo katika kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, hakukuwa na mabadiliko yoyote kwa upande wa mabao.
Wekundu wa Msimbazi sasa wamefikisha pointi 29, wakiishusha Azam FC katika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mkutano mdogo Simba waja
Kamati ya Uchaguzi ya Simba imesisitiza kuwa, rais mpya wa klabu hiyo atakayechaguliwa kwenye uchaguzi mdogo atakuwa chaguo la wana Simba na si vinginevyo.
Simba itafaya uchaguzi mdogo Februari 7 ili kuziba nafasi ya mwenyekiti, Swedi Mkwabi aliyejiuzulu mwaka jana.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Boniface Lihamwike alisema hakutokuwa na mchezo katika mchakato huo, akisisitiza kuwa utakuwa huru na wa haki.
“Atakayechaguliwa atachaguliwa kwa haki na wanachama wa Simba watampata kiongozi chaguo lao,” alisisitiza.
Moja ya sifa kubwa za mgombea wa nafasi hiyo, mbali ya kuwa Mtanzania, pia anapaswa kuwa mwanachama wa Simba kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu na mwenye elimu ya shahada ya kwanza inayotambuliwa na TCU na kila mgombea atalipia Sh300,000 ya fomu zinazoanza kutolewa leo hadi Desemba 24
Desemba 27 na 28 ni usaili, kutakuwa na siku nne za mapingamizi kuanzia Desemba 29 na Januari 5 hadi Februari 6 kitakuwa ni kipindi cha kampeni kwa wagombea wote waliopitishwa.
Alisema uchaguzi huo utaendeshwa chini ya kanuni za uchaguzi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwa katiba ya Simba inawaruhusu kufanya hivyo kwa kuwa klabu hiyo haina kanuni za uchaguzi.