Siri ya mafanikio ya kaseja kagera

Muktasari:
- Katika kipindi hicho, Kaseja ameiongoza Kagera kwenye mechi nne za mashindano tofauti, mbili za Ligi Kuu Bara na zingine Kombe za Shirikisho (FA) akishinda zote na kuifanya kuwa timu ya ushindani.
APRILI 4, mwaka huu, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja alitimiza mwezi mmoja tangu akabidhiwe timu hiyo akichukua mikoba ya Melis Medo aliyetimkia Singida Black Stars.
Katika kipindi hicho, Kaseja ameiongoza Kagera kwenye mechi nne za mashindano tofauti, mbili za Ligi Kuu Bara na zingine Kombe za Shirikisho (FA) akishinda zote na kuifanya kuwa timu ya ushindani.
Chini ya Kaseja, Kagera Sugar imefunga mabao manne na kuruhusu mawili kwenye mechi za ligi kuu huku ikipanda kwa nafasi moja kutoka 15 hadi 14 katika msimamo na kufufua matumaini ya kubaki kwenye michuano hiyo.
Kagera Sugar chini ya Kaseja kwenye michuano ya FA, ipo katika robo fainali baada ya kuifunga Namungo kwa mabao 3-0 hatua ya 32 bora na 16 bora iliiondosha Tabora United kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1.
Kwa sasa timu hiyo itakutana na Singida Black Stars katika robo fainali.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaseja alisema mafanikio anayoyapata yanatokana na wachezaji wake kumsikiliza na kumtazama kama kiongozi kutokana na wengi wao kucheza nao na wengine kufanya naye kazi akiwa kocha wa makipa kikosini hapo.
“Pongezi nyingi ziende kwa wachezaji wangu nafurahishwa na kila wanachokifanya. Wanafanya kwa moyo na wanapambana kuhakikisha Kagera Sugar inaendelea kucheza ligi msimu uja. Hili linawezekana kwa umoja wetu na namna ambavyo wamekuwa wakivuja jasho,” alisema na kuongeza.
“Nimefanya kazi na Kagera Sugar nikiwa kocha wa makipa kwa muda lakini pia kuna baadhi ya wachezaji nimecheza nao ligi moja, kitendo cha viongozi kunipa hii timu ni heshima kwangu lakini pia kwa wachezaji ambao wananifahamu hivyo tunazungumza na kukubaliana nini tufanye.”
Kaseja alisema bado wanaamini wana nafasi ya kufanya vizuri na kuibakiza Kagera Sugar icheze ligi msimu ujao sambamba na kucheza fainali Kombe la FA baada ya kutinga hatua ya robo huku akidai kuwa mapambano bado yanaendelea.