Straika Fountain Gate aomba muda

Muktasari:
- Nyota huyo alijiunga na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea JKU SC ya visiwani Zanzibar kwa lengo kuzipa pengo la mshambuliaji nyota wenzake, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco.
MSHAMBULIAJI wa Fountain Gate, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’ amesema licha ya kutoanza vizuri hadi sasa katika timu hiyo michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara, ila anaendelea kuzoea mazingira taratibu hivyo ni suala la muda.
Nyota huyo alijiunga na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea JKU SC ya visiwani Zanzibar kwa lengo kuzipa pengo la mshambuliaji nyota wenzake, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco.
“Jambo nzuri ni kuona kwanza timu yetu inafanya vizuri kisha hayo mengine yatafuata, kiukweli unapocheza michezo zaidi ya minne kwa mshambuliaji bila ya kufunga huwa inaumiza, ingawa hilo kwangu sijali ikiwa tutakuwa bora tukiwa uwanjani.”
Kwa upande wa Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano alisema kiu ya mshambuliaji yeyote ni kufunga ingawa ikitokea ukame wa aina hiyo huwa ni jambo la kawaida, japo anachokiangalia ni umuhimu na mchango anaoutoa kwa kushirikiana na wenzake.
Nyota huyo hadi sasa hajafunga bao lolote huku akitazamiwa kuzipa pengo la ‘Gomez’ aliyefunga mabao sita ya Ligi Kuu Bara, huku akitengeneza pacha kali ya ushambuliaji na mchezaji mwenzake, Edgar William mwenye mabao matano kikosini.
Akiwa na kikosi cha JKU SC, ‘Gonda’ alifunga mabao manane katika Ligi ya Zanzibar akiungana na washambuliaji wengine wa hivi karibuni walioibukia Bara, baada ya Seleman Mwalimu, Maabad Maulid wa Coastal Union na Yassin Mgaza wa Dodoma Jiji.