Tanzania, Cameroon patachimbika Morocco

Muktasari:
- Tanzania ilitinga nusu fainali kwa kumaliza kinara wa Kundi C baada ya mechi mbili kuvuna pointi nne, ikifuatiwa na Madagascar yenye mbili, huku Senegal ikiburuza mkia na moja.
TIMU ya taifa ya wanawake ya Futsal, leo Jumatatu itashuka Uwanja wa Sportif Prince Moulay Abdallah, huko Morocco kukipiga dhidi ya Cameroon katika mchezo wa nusu fainali ya mashindano ya mchezo huo kuwania Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.
Tanzania ilitinga nusu fainali kwa kumaliza kinara wa Kundi C baada ya mechi mbili kuvuna pointi nne, ikifuatiwa na Madagascar yenye mbili, huku Senegal ikiburuza mkia na moja.
Timu hiyo ilianza kampeni hizo kwa kutoa sare ya 4-4 na Madagascar mabao yaliyofungwa na Donisia Minja (mawili), Aisha Mnunka na Stumai Abdallah, kisha kuizima Senegal kwa mabao 3-1 yaliyofungwa na Donisia Minja, Vaileth Nicholas na Anna Katunzi.
Sasa inakutana na Cameroon ambayo katika mechi mbili imefunga mabao saba na kufungwa 12 kiufupi ukuta wa timu hiyo unapitika kama washambuliaji watakuwa makini, kwani ilianza kwa kupoteza 7-1 kwa Morocco, kisha ikaifunga Namibia kwa mabao 6-5 na kupata pointi tatu zilizoivusha nusu fainali.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, kocha wa Tanzania, Curtis Reid alisema; “Mechi mbili tulicheza kwa nidhamu kubwa tumejiandaa vizuri dhidi ya Cameroon na naamini wachezaji wataonyesha kiwango kikubwa.”
Kipa wa Tanzania, Naijat Abbas alisema; “Hii ndio mara yetu ya kwanza kushiriki huu mchezo naamini tutafika hadi fainali na kuchukua ubingwa.”
Wakati Tanzania ikitinga nusu fainali timu ya taifa ya Wavulana U15 imeibuka mabingwa wa mashindano ya Shule kwa Afrika, African Schools Football Championship (ASFC) kwa kuitoa Senegal kwa mikwaju ya penati 3-2 baada ya sare ya 0-0.