TP Mazembe: Simba imetushika pabaya

Kikosi cha timu ya TP Mazembe kilichoiangamiza timu ya Simba
MICHAEL MOMBURI SIMBA imewashika pabaya TP Mazembe. Mabingwa hao watetezi wa Afrika wamekiri kuwa bao la Emanuel Okwi hawakulitarajia na limewavurugia mahesabu. Mazembe ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Simba Jumapili iliyopita mjini Lubumbashi kwenye Uwanja wa Kenya ambapo timu hizo zitarudiana Aprili 2 jijini Dar es Salaam huku Simba ikihitaji kushinda mabao 2-0. Msemaji wa Mazembe, Jean Sidwe aliiambia Mwanaspoti jana Jumatatu kutoka Lubumbashi kwamba Simba iliwabana sana na hawakutarajia. “Simba ilicheza mpira sana muda wote, sema sisi tulifanya makosa ya kizembe kuruhusu bao moja, tumewapa faida na kufanya mchezo wa marudiano kuwa mgumu kwetu huko Dar es Salaam,”alisema Sidwe. “Tulitakiwa kushinda mabao mengi zaidi ya hayo tuliyopata halafu tusiruhusu goli ili mambo yawe rahisi na tulikuwa tunaweza kufanya hivyo, lakini mpira ndivyo ulivyo inabidi kujipanga sana kwa mechi ya marudiano.” “Simba wameonyesha kiwango cha juu, lolote linaweza kutokea kwenye mchezo wa marudiano, lakini tutajipanga vizuri tunajua cha kufanya na tumewaona, Simba vizuri,”alisisitiza. Rais wa Mazembe, Moise Katumbi amewaambia wachezaji kwamba; “Tunahitaji kupambana kufa na kupona kama tunataka kombe hilo kwa mara nyingine.” Kocha wa Mazembe, Lamine Nd’iaye amekiambia kituo kimoja cha redio mjini Lubumbashi kwamba mchezo wa Simba ni wa kasi lakini wachezaji wake wana uwezo wa kuwakabili na kusonga mbele. JERRY SANTO “Mazembe ni wazuri kwenye kucheza krosi lakini katika hawatishi sana, ndio maana uliona tulikuwa tunawamudu na tulisukuma mashambulizi, ni timu ambayo inafungika kabisa na tunaweza kufanya hivyo hapa Dar es Salaam. “Tunachopaswa kufanya ni kuongeza umakini kila idara na kucheza kwa malengo, tunawaweza,”alisisitiza kiungo huyo, Mkenya wa Simba jana Jumatatu. PATRICK KATALAY Mshambuliaji huyo mpya wa DC Motema Pembe, alisema ; “Nimesikitika sana kusikia Simba imefungwa mabao 3-1, niliwaambia mapema kwamba dakika 20 za kwanza Mazembe watakuja kwa kasi, wawazuie. Kilichotokea ndiyo kile kile Patou Kabangu na Ekanga wamefunga magoli mawili ndani ya dakika 21.” “Naamini Simba inaweza kuifunga Mazembe mabao 2-0 hapo Dar es Salaam, wakomae sana kwenye ulinzi na kujiamini, Simba wakiwa Dar es Salaam wanakuwa wakali sana naamini wataweza kuwatoa. Wawe makini ndani na nje ya uwanja kuanzia leo hii.” Uongozi wa Simba ulisema kuwa matokeo ya uwanjani si ya kutisha na walicheza vizuri na kwamba wanachofanya sasa ni kupanga mikakati ya mchezo wa marudiano.