Ushindi Mbeya City wampa mzuka Ambokile

Muktasari:
- Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, Ambokile alifunga bao moja katika ushindi huo na kufikisha mabao 10 katika Ligi ya Championship kwa msimu huu, huku mengine yakifungwa na Mudathir Said na Malack Joseph.
MSHAMBULIAJI wa Mbeya City, Eliud Ambokile amesema ushindi ilioupata kikosi hicho ugenini wa mabao 3-2, dhidi ya Geita Gold, umewapa matumaini makubwa ya kupambana michezo miwili iliyobaki ili kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, Ambokile alifunga bao moja katika ushindi huo na kufikisha mabao 10 katika Ligi ya Championship kwa msimu huu, huku mengine yakifungwa na Mudathir Said na Malack Joseph.
“Wapinzani wetu walitukamia sana kwa sababu kama unavyojua walikuwa na kampeni kubwa ya kuhakikisha wanatufunga kwao na kutupotezea malengo yetu, tunashukuru tulijipanga ipasavyo kukabiliana na hali hiyo na tulifanikiwa,” alisema Ambokile.
Ushindi huo umeifanya Mbeya City kuendelea kujikita nafasi ya pili na pointi 62, nyuma ya vinara Mtibwa Sugar iliyokata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku wapinzani wao wakubwa, Stand United ikiwa nafasi ya tatu na pointi 59.
Ambokile aliyeichezea Mbeya City tangu mwaka 2017, amecheza timu mbalimbali za, Black Leopards FC ya Afrika Kusini, TP Mazembe ya DR Congo na Nkana FC ya Zambia, huku akiipambania kuirejesha Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023.