Utamu kamili wa kikapu uko hivi

Muktasari:
- Kwanza wachezaji wanaotakiwa kucheza uwanjani ni watano, kati ya wachezaji 12 wanaoandikishwa kwa kila mchezo.
UNAUPENDA mchezo wa kikapu? Sasa hapa kuna mawili matatu kuhusu mchezo huo.
Kwanza wachezaji wanaotakiwa kucheza uwanjani ni watano, kati ya wachezaji 12 wanaoandikishwa kwa kila mchezo.
Tofauti na mchezo wa soka, ambako mchezaji akitoka haruhusiwi kurejea mchezoni, katika kikapu wachezaji wanaingia na kutoka.
Nafasi tano zinazochezwa na wachezaji hao katika kikapu ni ya point guard anayecheza namba 1, shooting guard (Na.2), small forward (Na.3), power forward (Na.4) na center (Na.5).
Wachezaji hawa huwa na majukumu tofauti uwanjani wakati wa mchezo, na pia mara nyingi huwa wanatofautiana hata katika maumbile kulingana na majukumu na maeneo ambayo huwa wanacheza.
Akielezea kuhusiana na majukumu ya kila mchezaji na nafasi zake, Kamishna wa Makocha wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Robert Manyerere anasema:
POINT GUARD
Jukumu lake la kwanza ni kupokea mipira yote inayoanzwa na kupeleka mpira upande wa pili kwa ajili ya mashambulizi.
Jukumu jingine alilonalo ni la kuongoza timu yake, katika mfumo wa kushambulia, pamoja na kutoa pasi kwa wafungaji.
SHOOTING GUARD
Mchezaji huyu anaweza kuwa karibu na mchezaji anayecheza nafasi ya point guard, wakati mwingine anaweza kuchukua majukumu ya kucheza nafasi hiyo.
Pamoja na kubeba majukumu hayo, anatakiwa kuwa mchezaji mwenye uwezo mzuri wa kufunga katika mitupo ya mbali.
SMALL FORWARD
Huyu ni mchezaji anayetakiwa kuwa na uwezo wa kukimbia kwa haraka na kufunga (fast break), kama ilivyo soka inakoitwa 'counter attack'.
POWER FORWARD
Anajulikana pia kama mchezaji wa nafasi ya chini (post player). Anapaswa kuwa ni mchezaji mweye nguvu zaidi, anacheza nafasi ya chini kupambana katika kufunga karibu na goli pamoja na kukamata mipira ya rebound.
CENTER
Huyu anatambulika kama mchezaji wa nafasi ya chini (post player), anatakiwa awe mchezaji mrefu zaidi, mwenye uwezo wa kuruka juu kufunga na kukamata mipira inayodunda na kurudishia (offensive rebound) au kuokoa (defensive rebound) kwa upande wake.