Mangungu atoa kauli Yanga kwenda CAS

Muktasari:
- Mangungu amezungumza hilo jana Ijumaa, katika mahojiano ya Mwananchi Digital mara baada ya ushindi wa Simba wa mabao 6-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa kiporo cha Ligi Kuu Bara
MWENYEKITI wa Simba SC, Murtaza Mangungu amegusia taarifa ya Klabu ya Yanga kuwa inataka kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), kudai pointi tatu za mchezo wa Kariakoo Dabi ambao uliahirishwa, akisema "hata wakienda sped" wao hawana hofu.
Mangungu amezungumza hilo jana Ijumaa, katika mahojiano ya Mwananchi Digital mara baada ya ushindi wa Simba wa mabao 6-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa kiporo cha Ligi Kuu Bara
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mangungu alionyesha ni kama kutokubaliana na Yanga kutafuta suluhu ya suala hilo huko CAS.
Alisema kuwa Yanga wana haki ya kutamani kile wanachotaka, lakini kwa upande wake, aliona kuwa hatua hiyo ni ya kupoteza muda.
"Kutamani ni sifa ya mwanadamu, anaweza kutamani kitu chochote. Hivyo, wacha waendelee kutamani. Sio CAS tu, hata wakienda Speed," amesema Mangungu.
Siku chache zilizopita Mwanaspoti iliripoti kuhusu viongozi wa Yanga kujiandaa kwenda CAS kwa ajili ya kudai pointi tatu za mchezo wa Kariakoo Dabi ambao uliahirishwa na kuelezwa na Bodi ya Ligi kuwa utapangiwa tarehe nyingine.
Ilikuwaje? Siku moja kabla ya mchezo huo wa Kariakoo Dabi, ambao ulitakiwa kuchezwa Jumamosi ya Machi 8, msafara wa Simba ulizuiwa kuingia uwanjani kwa ajili ya kufanya mazoezi. Hali hii iliwafanya viongozi wa timu hiyo kususia mchezo huo, huku wakieleza wasiwasi wao na kuandika barua rasmi kwa Bodi ya Ligi.
Bodi ya Ligi ilithibitisha kupokea barua hiyo na baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya Saa 72 iliamua kuahirisha mchezo huo. Hata hivyo, Yanga hawaonekani kukubaliana na uamuzi huo na walitoa taarifa wakisema kuwa hawapo tayari kucheza katika tarehe nyingine. Badala yake, walieleza wanachotaka ni pointi tatu za mchezo huo ulioahirishwa.