Wawili Prisons waisubiri Azam FC

Muktasari:

  • Pia habari njema kwa mashabiki wa Maafande hao ni kurejea kwa nyota wao wawili, Salum Kimenya aliyekosa mechi moja na Dotto Shaban ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu akiuguza nyonga.   

Kasi ya Tanzania Prisons kwenye mechi iliyopita imempa kiburi kocha mkuu wa timu hiyo, Ahmad Ally akitamba kuwa Azam nao lazima wapigwe nyingi.

               
Pia habari njema kwa mashabiki wa Maafande hao ni kurejea kwa nyota wao wawili, Salum Kimenya aliyekosa mechi moja na Dotto Shaban ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu akiuguza nyonga.   


Katika mechi iliyopita Prisons ikiwa katika ubora wake iliilaza Singida Fountain Gate mabao 3-1 na keshokutwa Jumapili watakuwa Sokoine kuwakaribisha Azam FC katika muendelezo wa Ligi Kuu.


Kwa upande wa Azam waliopo nafasi ya pili kwa alama 36 wanawakabili wapinzani hao waliopo nafasi ya saba kwa pointi 20 wakikumbuka suluhu ya bila kufungana dhidi ya Tabora United katika mchezo wao uliopita
Ally alisema timu hiyo imekuwa na muunganiko mzuri akibainisha anakoshwa na kasi ya straika wake kwa namna wanavyoelewana kwenye eneo la goli.


Alisema matokeo waliyopata kwenye mchezo uliopita wanahitaji kuyalinda na kuyaendeleza katika mechi ijayo dhidi ya Azam akitamba kuwa iwapo watajichanganya watakula nyingi.


Alisema wanafahamu Azam inao wachezaji wenye ubora akiwamo straika Prince Dube lakini kwa kikosi cha Prisons hawana hofu yoyote akisema kuwa mkakati wao ni mechi zote za Sokoine kubaki na pointi tatu.


“Tunajua ubora wa Azam na kasi ya Dube lakini tunajipanga maeneo yote kuhakikisha hapiti mtu na kama watajichanganya watapigwa nyingi, tunahitaji mechi zote za Sokoine tuvune pointi” alisema kocha huyo.