Yanga yatangulia fainali FA, ikiizima JKT TZ kibabe

Muktasari:
- Yanga ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga uliokuwa umejaa maji ya mvua zilizoufanya uwe na matope yaliyosababisha kupoteza utamu wa pambano hilo lililokuwa la kuvutia kwa namna timu zote zilivyocheza na kutengeneza nafasi nyingi zilizopotezwa na kila upande.
WATETEZI wa michuano ya Kombe la Kombe la Shirikisho (FA), Yanga jioni ya leo Jumapili, imeizima JKT Tanzania kwa kuichapa mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo na kutinga fainali, sasa ikisubiri mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Simba na Singida Black Stars.
Yanga ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga uliokuwa umejaa maji ya mvua zilizoufanya uwe na matope yaliyosababisha kupoteza utamu wa pambano hilo lililokuwa la kuvutia kwa namna timu zote zilivyocheza na kutengeneza nafasi nyingi zilizopotezwa na kila upande.
Ushindi huu wa Yanga unamaanisha kuwa sasa timu nne zinazoshiriki michuano ya CAF msimu ujao zimefahamika ambapo ni Simba na Yanga Ligi ya Mabingwa, huku Singida na Azam zikiwa kwenye Kombe la Shirikisho kwa kuwa timu itakayotwaa Kombe la FA ni kati ya zile nne bora za juu.
Katika mechi hiyo ya ushindani, ilishuhudia Yanga ikipata bao lililoipeleka fainali likifungwa na Prince Dube dakika ya 41, baada ya beki wa JKT Tanzania, Karim Mfaume kushindwa kuokoa mpira vizuri eneo la hatari na kumkuta mfungaji huyo.
Wakati timu hizo zikishambuliana kwa zamu, Yanga iliandika bao la pili lililofungwa na kiungo, Mudathir Yahya dakika ya 90, baada ya kupokea pasi safi iliyopigwa na Clatous Chama na kuuzamisha mpira wavuni uliomshinda kipa, Yakoub Suleiman.
Mechi hii ilikuwa ya kisasi kwa timu zote baada ya kushindwa kutambiana katika Ligi Kuu Bara mara ya mwisho zilipokutana Februari 10, 2025 na kutoka suhulu (0-0) ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi kikosini humo.
Hamdi aliyetangazwa na Yanga, Februari 4, 2025, akichukua nafasi ya Sead Ramovic aliyejiuzulu mwenyewe ili kwenda kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria na mechi hiyo ya JKT Tanzania ilikuwa ni ya kwanza kwake.
Yanga ilianza michuano hii ya FA hatua ya 64, kwa kuichapa Copco FC ya Mwanza mabao 5-0, kisha baada ya hapo ikakutana na Coastal Union hatua ya 32 na kuiondosha kwa kuifunga 3-1 na kutinga 16 bora na kuitoa Songea United ya Ruvuma mabao 2-0.
Katika hatua ya robo fainali, Yanga ikakutana na Stand United inayoshiriki Ligi ya Championship na kuichapa mabao 8-1, huku nyota wa timu hiyo, Stephane Aziz KI akifunga 'Hat-Trick', ikiwa ni ya kwanza msimu huu kwa mchezaji wa Ligi Kuu.
Kwa upande wa JKT ilianzia pia hatua ya 64 bora kwa kuitoa Igunga United ya Tabora kwa kuichapa mabao 5-1, kisha ikaitoa Biashara United inayoshiriki Ligi ya Championship kwa kuifunga 2-1, ikafuzu 16 bora na kuiondosha Mbeya Kwanza kwa 3-0.
Katika hatua ya robo fainali, kikosi hicho cha maafande kikafuzu na kwenda nusu fainali baada ya kutumia vyema Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambao ndio wa nyumbani kufuatia kuichapa Pamba Jiji FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa mabao 3-1.
Tangu michuano hiyo iliporejea tena msimu wa 2015-2016, Yanga ndio timu inayoongoza kwa kuchukua ubingwa huo mara nyingi zaidi, baada ya kufanya hivyo mara nne, ikifuatiwa na wapinzani wao wakubwa Simba, waliolichukua taji hilo mara tatu tu.
Simba itavaana na Singida BS Mei 31 katika mechi nyingine ya nusu fainali itakayopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo Babati, Manyara, hivyo endapo kikosi hicho cha Msimbazi kitashinda kitakutana na Yanga katika fainali ya 'Dabi ya Kariakoo', itakayovuta hisia za mashabiki.
Yanga imefuzu fainali ya tano mfululizo ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), tangu msimu wa 2020-2021, ambapo kati ya hizo imechukua ubingwa mara nne, huku ikikosa mara moja tu ilipochapwa na wapinzani wao Simba bao 1-0, msimu wa 2020-2021.
Tangu Yanga ikikumbane na kichapo hicho cha Simba, timu hiyo imechukua ubingwa wa michuano hiyo kwa mara tatu mfululizo, ikianza msimu wa 2021-2022, ilipoichapa Coastal Union kwa penalti 4-1, baada ya sare ya mabao 3-3, katika dakika 120.
Kwa misimu miwili mfululizo kuanzia 2022-2023 na 2023-2024, Yanga ikaichapa Azam FC bao 1-0, kisha ikashinda tena kwa mikwaju ya penalti 6-5, baada ya suluhu (0-0), mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Katika mchezo wa leo, Yanga itajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi mnono kwani nyota wa kikosi hicho akiwamo Stephane Aziz KI, Prince Dube, Maxi Nzengeli na Clement Mzize walipoteza nafasi nyingine za wazi, lakini hata JKT nayo ilifanya kosa kosa nyingine na kuinyima mabao ya wazi.