Mkenya afichua jambo Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga na Pamba Jiji katika dirisha dogo la Januari 2025, baada ya kuachana na Shabana FC ya kwao Kenya, amesema Ligi ya Tanzania ni ngumu na inayohitaji kupambana zaidi, ili uendelee kuonekana na kulitangaza jina lako pia.
MSHAMBULIAJI wa Pamba Jiji, Mkenya Mathew Momanyi Tegisi, amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja alichocheza Ligi Kuu Bara, ameona ushindani mkubwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo pia ndani ya timu hiyo na ugumu uliopo kwenye kila mechi.
Nyota huyo aliyejiunga na Pamba Jiji katika dirisha dogo la Januari 2025, baada ya kuachana na Shabana FC ya kwao Kenya, amesema Ligi ya Tanzania ni ngumu na inayohitaji kupambana zaidi, ili uendelee kuonekana na kulitangaza jina lako pia.
“Umekuwa mwaka mmoja wa mafanikio kwangu kupata changamoto mpya tofauti na sehemu niliyotokea, bado nina safari ndefu ya kuzidi kuonyesha makali yangu na kuisaidia timu kumaliza nafasi nne za juu kama ambavyo tunatarajia,” amesema Momanyi.
Akizungumzia kuhusu ushindani wa nafasi katika timu hiyo hususani eneo la ushambuliaji analocheza, Momanyi amesema kila mchezaji anapambana kwa ajili ya kushawishi benchi la ufundi, jambo ambalo linaongeza morali ya kuzidi kufanya vizuri.
Momanyi msimu wa 2024-2025, alifunga mabao saba katika Ligi Kuu, akiwa ndiye aliyeongoza kwa mabao ndani ya kikosi hicho.
Nyota huyo aliendeleza alipoishia akiwa na Shabana FC, kwa sababu kabla ya kujiunga na Pamba alikuwa pia amefunga mabao matano kwao Kenya, nyuma ya mshambuliaji mwingine wa kikosi hicho, Brian Michira, aliyekuwa anaongoza kwa kufunga saba.
Msimu huu wa 2025-2026, tayari nyota huyo amefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara akiwa ndiye anayeongoza ndani ya kikosi hicho, huku bao lake la mwisho, lilikuwa ni la ushindi wa 1-0 dhidi ya Namungo FC, Februari 10, 2026.