Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yona Amosi alivyoitikisa miamba ya Kariakoo

Muktasari:

  • Baada ya kuonyesha kiwango katika kuilinda milingoti yake mitatu kwa ustadi wa hali ya juu, Klabu kadhaa zilianza kumtumia ofa golikipa huyu ili kuinasa saini yake.

Kipa wa Pamba Jiji, Yona Amosi ni miongoni mwa walinda milango bora kwa sasa katika Ligi Kuu Bara akionesha mwendelezo wa makali yake anapokuwa kwenye milingoti mitatu, kiwango kilichozishawishi baadhi ya timu kwenye Ligi Kuu kutuma ofa ili kumnasa kipa huyo.

Yona ambaye pia ndio nahodha wa Pamba Jiji, alionesha kiwango kizuri msimu uliopita baada ya kumaliza na Cleen Sheet 11 akishika nafasi ya pili kwa magolikipa wazawa wakati namba moja alikuwa ni Patrick Munthali wa Mashujaa aliyemaliza na Cleen Sheet 12.

Msimu huu kipa huyu bado anaendelea kufanya vizuri ambapo hadi sasa amefikisha idadi ya Cleen Sheet tano akiwa nafasi ya nne sawa na Ally Salim wa Dodoma Jiji katika nafasi ya tatu wakati nafasi ya kwanza ikishikwa na Erick Johola wa Mashujaa mwenye Cleen Sheet sita sawa na kipa wa Yanga, Djigui Diarra anayeshika nafasi ya pili.


OFA ZILIVYOMWAGIKA

Baada ya kuonyesha kiwango katika kuilinda milingoti yake mitatu kwa ustadi wa hali ya juu, Klabu kadhaa zilianza kumtumia ofa golikipa huyu ili kuinasa saini yake.

Wakati tetesi za usajili za kunyemelewa na vigogo Simba na Yanga zikizidi kushika kasi, kipa huyo tegemeo wa Pamba Jiji, inadaiwa hakuripoti kambini jijini Mwanza ambako timu hiyo ilikuwa ikiendelea na mazoezi wakati wa dirisha dogo la usajili.

Pamba ilirejea kambini tangu Desemba 29, mwaka jana ikijifua kwenye Uwanja wa Nyamagana kujiandaa na mwendelezo wa Ligi Kuu Januari 21 baada ya kusimama karibu mwezi mzima kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yaliyofanyika huko Morocco.

Yona aliyehusishwa na Simba na Yanga zilizokuwa zikisaka makipa kupitia dirisha dogo, alikosekana katika mazoezi ya timu hiyo akiwa mmoja ya wachezaji ambao hawakuripoti kambi ya timu hiyo kwa wakati, huku kuchelewa kwake kukihusishwa na dili hilo la kutaka kujiunga na vigogo hao waliokuwa kwenye Kombe la Mapinduzi 2026.

Licha ya dau zuri alilowekewa mezani na Yanga ili kuvaa jezi ya njano na kijani msimu huu, kipa huyu wa Pamba Jiji, alishindwa kujiunga na timu hiyo huku ikielezwa ameukwepa mziki wa Djigui Diarra.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga, kilieleza kuwa, kilichowakwamisha kupata saini ya kipa huyo ni mwenyewe kuhitaji nafasi ya kucheza mara kwa mara kama ilivyo Pamba Jiji, kitu ambacho sio rahisi bila ya kupambania namba dhidi ya Diarra na Aboutwalib Mshery.

“Ni kweli tuliwekeza juhudi za kumpata kipa huyo na kuweka dau zuri mezani, lakini tumekwama katika kipengele cha kumhakikishia nafasi ya kucheza, kwani hilo linatokana na uwezo wake uwanja wa mazoezi akilishawishi benchi la ufundi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Yona amesema anaamini katika kukuza kipaji chake kwa kucheza kama ilivyo Pamba Jiji, hivyo ili aweze kutua katika kikosi chetu pia apate hiyo nafasi sio rahisi kwani timu tayari ina kipa namba moja na mbili, hivyo juhudi zake ndizo zingeshawishi benchi na sio sisi kumhakikishia.”

Kwa mujibu wa chanzo, Yanga ilimwekea Yona dau la Sh100 milioni na mkataba wa miaka miwili, lakini kitendo cha kutaka kucheza mara kwa mara, ikafanya dili hilo lishindikane.

Chanzo hicho kilipoulizwa ni kwa nini walimtaka kipa huyo wakati tayari wana makipa watatu Diarra, Mshery na Khomeiny Abubakar, kilisema Khomeiny anakaribia kumaliza mkataba lakini pia anasumbuliwa na majeraha.

“Tulikuwa tunapambana na Yona baada ya kubaini kipa wetu namba tatu ana majeraha na mkataba wake pia unamalizika, tulihitaji kipa atakayeongeza ushindani wa namba na kuongeza ubora wa makipa wengine,” kilisema chanzo hicho kutoka Yanga.

“Baada ya kukosa saini ya Yona akili kubwa ikatumika na kuamua kumalizana na Hussein Masalanga, tunaamini pia ni kipa sahihi kwa wakati huu,” kiliongeza.

Masalanga alitua Yanga kwa mkataba wa miezi sita akiwa ametoka kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 akiwa na Taifa Stars iliyoishia hatua ya 16 Bora kwa kutolewa na wenyeji Morocco waliopoteza mechi ya fainali mbele ya Senegal.

Yona aliyewahi kuidakia Tanzania Prisons amekuwa alihusishwa na Yanga tangu msimu uliopita kabla ya kuibukia Pamba Jiji na wakati wa dirisha dogo alirejea katika vichwa vya habari akitakiwa na timu hiyo sambamba na Simba ambayo makipa wake wawili, Yakoub Suleiman na Moussa Camara wote walikuwa majeruhi wa muda mrefu.

Hadi sasa Yona amechangia kuisaidia Pamba Jiji kuvuna pointi 24 ikishika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu sawa na Azam FC ambayo inashika nafasi ya nne na Simba iliyopo nafasi ya tatu.

Pamba jiji imecheza jumla ya mechi 15 za Ligi Kuu Bara, ikishinda mechi sita, imetpata sare mechi sita na kupoteza mara tatu huku ikifunga mabao 14 huku yenyewe ikiruhusu 15.


AMEKUWA MFANO WA KUIGWA

Nyanda wa Coastal Union, Wilbol Maseke alimtaja Yona Amosi kuwa anapaswa kutazamwa kwa jicho la ziada, huku akiweka wazi ana kipaji kikubwa.

Mbali ya Yona Maseke pia alimtaja kipa wa Yanga, Djigui Diarra kuwa ni sehemu ya makipa ambao amekuwa akiwatazama na kujifunza kutoka kwao.

“Napenda kujifunza na kutazama makipa ambao wamekuwa wakinipa changamoto ya ushindani Diarra na Yona ni makipa ambao nimekuwa nikiwaangali ni wazuri sana wakiwa langoni wanafahamu majukumu yao. Diarra anapenda kucheza kwa miguu zaidi ya mikono ni kipa wa kisasa na mimi huwa napenda kufanya hivyo.”

“Diarra ni kipa mwenye mafanikio makubwa na anathaminiwa na nchi yake. Anayoyafanya Yanga, anayafanya mara mbili zaidi kwa timu yake taifa ya Mali. Nchi yake inathamini anachokifanya, natamani hilo litokee pia kwa Yona, ni kipa mzuri sana ana kila sababu ya kuitwa Stars.”

Maseke alisema, Yona ukiondoa ubora, namba zake pia zinambeba kuwa sehemu ya kikosi cha Stars kwani kwa misimu miwili mfululizo ameonyesha ubora akiwa na Pamba Jiji akiwa panga pangua kikosi cha kwanza, hivyo anapaswa kupewa heshima yake.

“Mimi siyo msemaji wake wala sio kwa ubaya, wanaoitwa Stars ni wazuri, naye pia anastahili kutokana na namba zake.”

Kwa upande wa Yona, bado anaendelea kuonesha kiwango bora katika kikosi hicho kinachoongozwa na kocha Francis Baraza huku macho na masikio ya mashabiki wengi yakisubili kuona na kusikia hatma ya nyota huyo wa Taifa Stars kama ataondoka au ataendelea kubakia Pamba Jiji.