Prime
Tahadhari yatolewa Yanga!
YANGA imetambulisha mashine tatu za kimataifa kwa mpigo, huku ikisema imebakisha nafasi mbili ili kuwa tano ambazo zitakwenda kuungana na zile saba zilizochangia kupatikana ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita.
Mashine hizo tatu zilizotambulishwa usiku wa Julai 24, 2026 na rais wa klabu hiyo, Hersi Said ni mshambuliaji Cheikh Ibrahima Toure na viungo washambuliaji Albert Kangwanda na Housseine Zakouani.
Sasa wakati mashabiki wa Yanga wakisubiri kuziona mashine hizo zikianza kazi ya kupigania mafanikio ya klabu hiyo kwa msimu wa 2026-2027, kocha mmoja aliyewahi kufundisha ndani ya timu hiyo, ametoa tahadhari kwa wapinzani akisema wanapaswa kujipanga kwani kuna vyuma hapo hatari.
Kocha aliyeyasema hayo ni Mzambia, George Lwandamina, aliyeinoa Yanga kuanzia Oktoba 24, 2016 hadi Aprili 9, 2018 ambapo kwa kina alimchambua Mzambia mwenzake, Kangwanda akisema ni mchezaji sahihi kutua klabuni hapo na kutokana na ubora wake, anaweza kufanya vizuri zaidi, hivyo kuna kila sababu wapinzani kujipanga kumkabili endapo tu akizoea mapema mazingira.
Lwandamina ambaye amewahi pia kuifundisha Azam kuanzia Desemba 3, 2020 hadi Juni 30, 2021, amesema Kangwanda ni mchezaji mwenye ufundi mkubwa ambaye ataweza kuipa kitu tofauti timu hiyo kutokana na ubora wake wa kujua kutengeneza nafasi na hata kufunga.
“Ndio namjua Kangwanda ni kijana wetu hapa Zambia, ana kipaji kikubwa, anaweza sana kushambulia akitokea pembeni, inategemea kocha anataka kumtumiaje kwenye mifumo yake,” amesema Lwandamina ambaye kwasasa anaifundisha timu ya taifa ya Zambia akichukua majukumu hayo kwa muda tangu Machi 2026 kufuatia kuondoka kwa Moses Sichone.
“Anajua sana kutumia mguu wa kushoto, anaweza kufunga na kutengeneza nafasi, nadhani (Yanga) wamepata mchezaji mzuri, anatakiwa tu apambane, naijua Ligi ya Tanzania sio rahisi sana lakini akijituma kila kitu kinawezekana. Kama atafanikiwa kuingia kwenye mfumo, bila shaka wapinzani wanapaswa kujipanga kumkabili.”
Wakati Lwandamina akizungumzia hivyo kuhusu Kangwanda, kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ naye akamchambua Cheikh Ibrahima Toure akisema Yanga wamepata mshambuliaji sahihi.
Robertinho aliyeinoa Simba kuanzia Januari 3, 2023 hadi Novemba 9, 2023, amesema anamjua Toure ambaye alikuwa akiitumikia Al Jabalain ya Saudi Arabia, akisema mshambuliaji huyo ni mjuzi wa kutumia nafasi ambaye anapenda kucheza kwa hesabu nyingi uwanjani.
Robertinho ambaye kwasasa anaifundisha Jeddah SC ya Saudi Arabia, amesema Toure kama atapata viungo wazuri wa kumtengenezea nafasi, anaweza kuwa tishio kwenye Ligi ya Tanzania kutokana na uwezo wake wa kufunga kwa kichwa na hata miguu.
“Yanga wamempata Cheikh Toure? Ni mchezaji mzuri, namfahamu anacheza nafasi ya ushambuliaji, hapo wamepata mshambuliaji mzuri wa daraja la juu, kama bado (Yanga) wana viungo wazuri basi watafurahia kazi nzuri kutoka kwake,” amesema Robertinho ambaye kipigo cha mabao 5-1 wakati akiwa Simba Novemba 5, 2023, kilichangia kusitisha mkataba wake.
Kocha huyo ameongeza: “Anajua kufunga kwa kichwa lakini anaweza kufunga kwa miguu, ana akili sana anapokuwa karibu na goli la wapinzani, nimemuona sana hapa Saudi Arabia.”
Hata hivyo, Robertinho amemuonya mshambuliaji huyo akisema hata kama anatoka kwenye Ligi ya juu nchini Saudi Arabia lakini anatakiwa kujipanga kwani Ligi ya Tanzania sio rahisi.
“Ninachoweza kusema anatakiwa kujiandaa kucheza ligi nyingine ngumu zaidi, hapa Saudi ndio Ligi ipo juu lakini Tanzania kuna Ligi ngumu pia, hapo wanatumia sana nguvu kwenye mechi nyingi na hata viwanja vingi sio kama hivi vya hali ya juu huku Saudia.
“Anatakiwa kujiandaa na akili yake kwamba anatakiwa kupambana, haitakuwa rahisi sana kwake, anakwenda kuchezea timu yenye mashabiki wengi, akianza vizuri itamjenga,” amesema kocha huyo raia wa Brazil.