Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba Queens yamnasa Mhabeshi

MHABESHI Pict

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo wa zamani wa CBE ya Ethiopia amejiunga na Simba Queens kwa mkataba wa mwaka mmoja na alikuwa akihusishwa pia na Yanga Princess.

BAADA ya zaidi ya mwaka mmoja wa kumfuatilia, kusubiri na kupambana na changamoto za taratibu za usajili, hatimaye Simba Queens imenasa saini ya kiungo wa kimataifa wa Ethiopia, Senaf Wakuma.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa CBE ya Ethiopia amejiunga na Simba Queens kwa mkataba wa mwaka mmoja na alikuwa akihusishwa pia na Yanga Princess.

Taarifa inaeleza Simba ilianza harakati za kumfuatilia tangu dirisha lililopita na alikuwa tayari kusaini mkataba na mabingwa hao, hata hivyo, dili hilo lilikwama dakika za mwisho baada ya Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutokamilika kwa wakati kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Baada ya dili hilo kuvunjika, Wakuma alirejea nchini Ethiopia na kusaini mkataba wa muda mfupi na klabu yake ya Mechal, lakini msimu wake haukuwa mzuri kutokana na majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.

Sasa baada ya kumaliza mkataba wake na kupona majeraha, inaelezwa Simba imeshakamilisha taratibu zote za usajili na muda wowote kuanzia sasa atatangazwa.

"Ni kweli kulikuwa na vitu wanakamilisha na kuna timu nyingine ilikuwa inamtaka lakini ofa nzuri aliyopata kutoka Simba imemfanya asaini mkataba," kilisema chanzo hiko na kuongeza

"Hata hivyo Simba inacheza michuano ya CAF hilo nalo limemvutia kujiunga na mabingwa hao ambao wana rekodi nzuri kwenye mashindano hayo."

Nyota huyo anatua Msimbazi akiwa na rekodi nzuri katika soka la wanawake Ethiopia na aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2024/25, huku pia akiibuka mfungaji bora wa michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) ukanda wa CECAFA akiweka kambani mabao sita.

Wakuma anakuja Simba kuziba nafasi ya mshambuliaji Zawadi Usanase, ambaye amepewa mkono wa kwaheri baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa msimu mmoja. Nyota huyo kutoka Rwanda alimaliza msimu akiwa amefunga mabao saba, lakini viongozi wa Simba wameamua kufanya mabadiliko wakiamini Mhabeshi anaweza kuongeza kitu kikubwa katika safu ya ushambuliaji kuelekea mashindano ya ndani na kimataifa.

Mbali na Wakuma Simba inatajwa kumalizana na mshambuliaji Mabinty Camara, akijiunga na mnyama akitokea Determine Girls FC ya Liberia kwa mkataba wa miaka miwili.

Camara anajiunga na Simba akichukua nafasi ya Mkenya Cynthia Shilwatso ambaye hakuanza msimu vizuri akikumbana na majeraha pamoja na Ernestine Heutchou raia wa Cameroon ambao walipewa mkono wa kwaheri.

Camara alimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa ligi akifunga mabao 23, huku akitwaa tuzo yake ya tatu ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Liberia.

Akizungumzia hilo, Mratibu wa Simba Queens, Selemani Makanya, amesema ni mpango mkakati wa timu kufanya maboresho machache na kuongeza wachezaji wapya kuelekea kwenye mashindano makubwa ya Afrika.

“Msimu uliopita ulikuwa wa kutengeneza timu na tayari imepata muunganiko, hivyo tumezungumza na kocha Mgosi na ametuelekeza mabadiliko madogodogo tu ya kuyafanya na tayari tumeyafanyia kazi,” amesema Makanya.