Ancelotti, Real Madrid siku zinahesabika, asubiriwa Brazil

Muktasari:
- Kocha Dorival Junior, alitimuliwa na Brazil baada ya kula kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Argentina kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia.
Madrid Hispania. Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti anatarajiwa kuondoka kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Carlo Ancelotti alirejea kwenye kikosi cha Real kwa mara ya pili na anatarajiwa kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu huku akitajwa kuwa anaweza kuchukua timu ya Taifa ya Brazil.
Mkataba wa Ancelotti na timu hiyo ya Bernabeu itamalizika mwishoni mwa mwakani, lakini inaelezwa kuwa makubaliano ya pande zote mbili yameshafikiwa na kocha huyo mwenye mafanikio makubwa ataondoka baada ya michezo mitano ijayo.
Madrid ilichapwa mabao 3-2 juzi na Barcelona kwenye fainali ya Copa del Rey lakini pia ikiwa imeshatupwa nje kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilipotolewa na Arsenal mwanzoni mwa mwezi huu.
Kwa sasa timu hiyo ipo pointi nne nyuma ya Barcelona kwenye msimamo wa La Liga huku kukiwa na michezo mitano ambayo ndiyo inaweza kuwa muhimu zaidi kwa timu hiyo kwani haina uhakika wa kombe lolote msimu huu.
Vyanzo vinasema kuwa kocha huyo anatakiwa na timu ya Taifa ya Brazil na ataanza kazi yake mwishoni mwa msimu huu akiwa anatakiwa kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia.
Kocha Dorival Junior, alitimuliwa na Brazil baada ya kula kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Argentina kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia.
Ancelotti anatarajiwa kuwa kocha wa Brazil kabla ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Ecuador na Paraguay Juni mwaka huu. Mchezaji wa zamani wa Real Madrid, Xabi Alonso ambaye kwa sasa anaifundisha Bayern Leverkusen anatajwa kuwa na nafasi ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 65.