Arsenal yatua kwa Rodrygo

Muktasari:
- Taarifa za awali zinaeleza kwamba Rodrygo amekuwa akifikiria kuondoka Real Madrid kwa ajili ya kujiunga na timu itakayompa heshima na nafasi kubwa zaidi ya kucheza tofauti na ilivyo timu hiyo ambapo anaona hapati heshima anayostahili.
ARSENAL imeonyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Rodrygo Goes katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi ili kuboresha eneo la ushambuliaji.
Taarifa za awali zinaeleza kwamba Rodrygo amekuwa akifikiria kuondoka Real Madrid kwa ajili ya kujiunga na timu itakayompa heshima na nafasi kubwa zaidi ya kucheza tofauti na ilivyo timu hiyo ambapo anaona hapati heshima anayostahili.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil, mkataba wake na Real Madrid unatarajiwa kumalizika Jun 30, 2028 na haijaelezwa ikiwa timu hiyo itakuwa tayari kumuachia.
Katika msimu uliopita, Rodrygo amecheza mechi 51 za michuano yote akifunga mabao 14 na kutoa asisti 10.
Hata hivyo supastaa huyo anadaiwa kutaka kuzungumza kwanza na kocha mpya, Xabi Alonso kabla ya kuamua ikiwa ataondoka au la.
Tangu alipowasili Kylian Mbappe katika kikosi cha Real Madrid, nafasi ya Rodyrigo katika kikosi cha kwanza cha wababe hao wa Jiji la Madrid imekuwa ndogo na kusababisha uibuke uvumi mwingi juu ya hatima yake.
Hata hivyo, licha Arsenal kuonekana kupewa nafsi kubwa ya kumsajili mchezaji huyo, lakini zipo pia timu kibao kutoka Ligi Kuu England ( EPL) na Hispania (LaLiga) zinazofuatilia kwa karibu kile kinachoendelea juu yake.
Matt O’Riley
EVERTON inaonyesha nia ya kumsajili kiungo wa Brighton, Matt O’Riley, mwenye umri wa miaka 24, lakini haina uhakika kama timu yake itakuwa tayari kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark. Tangu kuanza kwa msimu uliopita amecheza mechi 29 za michuano yote na kufunga mabao mawili. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2029.
Pedro Goncalves
MANCHESTER United inataka kumsajili kiungo wa kati wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Ureno, Pedro Goncalves, 26, kama mbadala wa kiungo mwenzake wa Ureno, Bruno Fernandes, 30, iwapo ataondoka kwenda Saudi Arabia katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi. Pedro ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha viwango bora katika kikosi cha Lisbon hususan msimu uliopita.
Marc Guehi
MABOSI wa Newcastle United wako tayari kuanza mchakato wa kufanya usajili wa kikosi dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi kwa kutuma ofa kwenda Crystal Palace ili kuipata saini ya beki kisiki wa timu hiyo na England, Marc Guehi, 24, pamoja na mshambuliaji wa Brentford na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo mwenye umri wa miaka 25.
Nahuel Molina
NEWCASTLE United ipo katika hatua nzuri za mazungumzo na Atletico Madrid juu ya beki wa kulia wa timu hiyo, Nahuel Molina ambaye pia anawindwa na Napoli, Juventus na Roma. Molina, 27, ameonyesha kiwango bora msimu uliopita na mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote.
Antony
KOCHA wa Bayer Leverkusen, Erik ten Hag, amewasilisha jina la winga wa Manchester United, Antony mwenye umri wa miaka 25, ambaye alimsajili alipokuwa akiifundisha Old Trafford baada ya awali kufanya naye kazi wakiwa Ajax. Inaelezwa Ten Hag bado ana imani na Antony na ameonyesha kuvutiwa zaidi baada ya kiwango bora alichoonyesha akiwa na Real Betis msimu uliopita.
Joao Palhinha
KIUNGO wa kati wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ureno, Joao Palhinha, ambaye amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, bado anatamani kuendelea kusalia kwenye viunga hivyo. Palhinha, 29, anaamini bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kucheza kwenye kikosi cha mabingwa hao wa Bundesliga.
Matheus Fernandes
ASTON Villa, West Ham United na Leeds United zimeanza mazungumzo na Southampton kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa timu hiyo na timu ya taifa ya Ureno, Matheus Fernandes, 20. Fernandes ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029, msimu uliopita amecheza mechi 43 za michuano yote na kufunga mabao matatu.