Beki Maguire akiri kumtuliza Zirkzee
Muktasari:
- Fowadi Zirkzee, ambaye alijiunga na Man United kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana akitokea Bologna, alicheza kwa kiwango cha hovyo sana katika mechi hiyo ya Newcastle na kutolewa katika dk33 tu ya mchezo na kukutana kelele za kuzomewa na mashabiki katika kipute hicho cha kichapo cha mabao 2-0 uwanjani Old Trafford, Desemba 30 mwaka jana.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI, Harry Maguire amesema kwamba bado anajihesabu kama mchezaji kiongozi kwenye kikosi cha Manchester United akifichua namna alivyomrudisha kwenye hali nzuri straika Joshua Zirkzee baada ya kukumbana na kelele za kuzomewa na mashabiki wa timu hiyo katika mechi dhidi ya Newcastle.
Fowadi Zirkzee, ambaye alijiunga na Man United kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana akitokea Bologna, alicheza kwa kiwango cha hovyo sana katika mechi hiyo ya Newcastle na kutolewa katika dk33 tu ya mchezo na kukutana kelele za kuzomewa na mashabiki katika kipute hicho cha kichapo cha mabao 2-0 uwanjani Old Trafford, Desemba 30 mwaka jana.
Mdachi huyo alitoka uwanjani akimwaga machozi, lakini Maguire, ambaye ni nahodha wa zamani wa United alitumia ukomavu wake kumtuliza Zirkzee.
“Nilimtumia meseji baada ya ile mechi ya Newcastle,” alisema Maguire kabla ya mechi dhidi ya Rangers, juzi Alhamisi.
“Sikia, Joshua ni mchezaji mzuri - huwezi kucheza kwenye klabu hiyo kama sio mchezaji mzuri. Tuna mashabiki wa aina yake ambao wamekuwa nasi kwenye nyakati zote nzuri na mbaya. Sio ishu ya ubinafsi.”
Katika mechi iliyofuatia, sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool, Zirkzee alishangiliwa na mashabiki wa Man United wakati anatolewa dakika 86, kisha alikwenda kufunga penalti muhimu wakati Man United ilipoitupa nje Arsenal kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA.
Maguire alikuwa nahodha wa United kwa miaka mitatu na nusu kabla ya kuvuliwa na Erik ten Hag.
“Nimekuwa mzoefu sasa, nimecheza kwenye klabu hiyo kwa nyakati zote za kupanda na kushuka. Nilikuwa nawatazama wachezaji waliopita kama Wayne Rooney na (David) Beckham, walikuwa na msaada mkubwa kwa wenzao na hilo liliwafanya kuwa wachezaji wakubwa.”