Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Brazil 2014: Brazil inaanza na vita ya wakali hawa kwenye tuzo ya Mchezaji Bora

Muktasari:

Tuachane na hilo, wakati fainali hizo zikianza rasmi usiku wa leo, mastaa kibao waliopo kwenye michuano hiyo wataingia uwanjani kuonyesha viwango bora vya kuyasaidia mataifa yao, lakini pili ni kusaka nafasi ya kunyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano (Golden Ball).

HATIMAYE siku imefika. Leo Alhamisi, mwamuzi Mjapani, Yuichi Nishimura, atapuliza kipyenga kuanzisha mechi ya ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia wakati wenyeji Brazil watakaposhuka kwenye Uwanja wa Itaquerao mjini Sao Paulo kumenyana na Croatia. Ni mechi ya kwanza kabisa ya fainali za Kombe la Dunia 2014.
Refa Nishimura atasaidiwa na Wajapani wenzake, Toru Sagara na Toshiyuki Nagi, huku mwamuzi wa akiba akiwa ni raia wa Iran, Alireza Faghani.
Kwenye fainali zilizopita za Kombe la Dunia mwaka 2010 kule Afrika Kusini, Nishimura alichezesha mechi nne, ikiwamo ya Brazil ilipochapwa 2-1 na Uholanzi kwenye hatua ya robo fainali, mchezo ambao Brazil ilimaliza pungufu baada ya kiungo, Felipe Melo kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye dakika ya 73 kwa kumchezea vibaya Arjen Robben.
Je, Nishimura atakuwa na bahati na Brazil mwaka huu au ataendelea kuwa mwamuzi asiyekuwa na bahati kwa Wabrazili? Tusubiri tuone.
Tuachane na hilo, wakati fainali hizo zikianza rasmi usiku wa leo, mastaa kibao waliopo kwenye michuano hiyo wataingia uwanjani kuonyesha viwango bora vya kuyasaidia mataifa yao, lakini pili ni kusaka nafasi ya kunyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano (Golden Ball).
Mesut Ozil
Kiungo mchezeshaji, Mjerumani aliyeanza kwa kasi kisha akapoa wakati anaanza kuichezea Arsenal mwaka jana, lakini anaweza kuwa msaada mkubwa kwa timu ya taifa ya Ujerumani kwenye fainali hizo.
Kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizopita nchini Afrika Kusini, Ozil alichaguliwa kuchuana kwenye tuzo ya Mchezaji Bora, mwaka huu nchini Brazil inaweza kuwa nafasi yake ya kufanya mambo makubwa zaidi na kuibuka kidedea. Ndiye mtu anayewapa uhakika Ujerumani katika kutesa kwenye fainali hizo.
Thiago Silva
Kwa miaka mingi, Brazil imekuwa ikitawaliwa na washambuliaji na ndiyo mara nyingi wanaotajwa kutamba, lakini kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu mambo yamebadilika.
Beki mwenye hadhi kubwa kwa sasa duniani, Thiago Silva, anapewa nafasi ya kung'ara na kikosi hicho cha Brazil kwenye fainali hizo na kuwekwa kwenye orodha ya wakali wanaopewa nafasi ya kuwa wachezaji bora wa michuano hiyo.
Brazil haiwezi kumshinda kila mtu kwenye fainali hizo, lakini kwa kuwa na beki huyo kikosini kwao wanakuwa na imani kubwa kwamba wana ukuta imara utakaowafanya wawe na uhakika wa kushinda mechi kwa sababu beki yao haitapitika kirahisi. Beki wa Italia, Fabio Cannavaro alifanya hivyo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006.

Andres Iniesta
Kiungo Mhispaniola, Andres Iniesta, alifunga bao matata kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2010 dhidi ya Uholanzi na kuipa Hispania ubingwa wa Dunia.
Nyota huyo anayecheza kwenye klabu ya Barcelona, imekuwa kawaida yake kung'ara kwenye michuano mikubwa. Aling'ara kwenye Euro 2008, Kombe la Dunia 2010, Euro tena 2012 na sasa anasubiri kuonyesha makali yake kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia.
Mhispaniola huyo si mfungaji wa mabao mengi, lakini amekuwa akitoa pasi hatari zinazoisaidia timu yake kushinda na ndiye mchezaji anayeweza kudumu zaidi mfumo unaotumiwa na Hispania wa kupiga pasi nyingi fupi fupi 'tika-taka'.
Bastian Schweinsteiger
Wajerumani wanakwenda Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia wakiwa na kikosi chenye viungo makini watupu. Kwenye safu hiyo ya kiungo ambacho ni muhimu kwa mfumo wa soka la kisasa, Ujerumani itaongozwa na mkali wake, Bastian Schweinsteiger.
Kwenye soka la kisasa, timu inaweza kushinda au kushindwa na kila kitu juu ya mambo hayo kinafanywa kwenye kiungo. Staa huyo anayecheza soka kwenye klabu ya Bayern Munich, ni mtu anayependa kutawala sehemu ya katikati ya uwanja. Kwa kulifanya hilo kutampa nafasi ya kuonyesha mambo makubwa nchini Brazil na kumweka kwenye wakati mzuri wa kuwa mchezaji bora wa michuano.
Eden Hazard
Mmoja wa wakali wanaounda kizazi cha dhahabu cha Ubelgiji kwa sasa. Uwezo wa soka lake unampa nafasi kubwa ya kuzoa mashabiki kwenye fainali hizo. Huyu ni Eden Hazard, staa wa Chelsea ambaye uwepo wake kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia unaweza kumpa hadhi kubwa baada ya michuano hiyo.
Winga huyo mwenye kipaji kikubwa cha mpira, amelionyesha hilo kwenye kikosi cha Chelsea msimu uliopita na sasa atakwenda Brazil kwa dhamira moja tu kuionyesha Dunia uwezo wa miguu yake inapokuwa na mpira na huu ni wakati wake wa kwenda kufanya mambo makubwa kwenye fainali hizo za Brazil.

Cristiano Ronaldo
Staa wa Ureno, Cristiano Ronaldo, atakwenda kwenye fainali hizo akiwa mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka (Ballon d'Or) hukua akiwa pia amenyakua medali ya ushindi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi chake cha Real Madrid.
Mwanzoni alizua hofu juu ya afya yake, lakini sasa amerejea uwanjani kwenye mechi ya kirafiki na kuonyesha kiwango kinachotoa matumaini kwamba hatashikika kwenye fainali hizo za Brazil.
Uzuri uliopo ni kwamba fainali hizo zitawashirikisha wapinzani wake wote wakubwa kwenye kizazi hiki cha sasa na baada ya kuisaidia nchi yake kunyakua tiketi ya kucheza michuano hiyo mbele ya Sweden,  Ronaldo anatabiriwa kwenda kutesa kwenye fainali hizo.
Neymar
Akiwa na umri wa miaka 22, Neymar anakuwa mtu tofauti sana anapokuwa ndani ya jezi za Brazil kuliko anapokuwa na za Barcelona. Kwenye kikosi cha Barcelona staa huyo pengine bado hajafanya makubwa, lakini siku anapotinga uzi wa rangi ya manjano na kijani, anakuwa hatari.
Alifanya hivyo kwenye Kombe la Mabara mwaka jana wakati michuano hiyo ilipofanyika kwenye ardhi ya nchi hiyo na sasa atabeba majukumu makubwa ya Brazil kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia kwa kuanzia na mchezo wa leo wa ufunguzi dhidi ya Croatia.
Kutokana na kile alichokifanya kwenye Kombe la Mabara, Neymar anabeba imani ya Wabrazili waliowengi kwamba atawafanya watese kwenye mikikimikiki hiyo.
Lionel Messi
Anatuzo nne za ubora duniani alizonyakua kutokana na umahiri wake wa uwanjani na mafanikio aliyopata akiwa na kikosi cha Barcelona. Kwenye timu ya taifa, Lionel Messi, bado hajafanya jambo kubwa, huku wataalamu wa soka wakiamini kwamba fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu nchini Brazil ni zamu yake kutamba.
Messi atakwenda kwenye michuano hiyo akiwa na nia moja ya kuyafikia mafanikio ya Diego Maradona aliyofanya na Argentina kwenye Kombe la Dunia mwaka 1986.
Msimu uliopita hakuwa kwenye ubora wake, lakini wengi waliamini kwamba alikuwa akitunza nguvu kwa ajili ya fainali hizo za Kombe la Dunia. Kocha wa Argentina, Alejandro Sabella amefichua wazi kwamba staa huyo ndiye tumaini lake kubwa kwenye mikikimikiki hiyo kwamba atazisumbua sana timu pinzani.
Nyota wengine
Kwenye orodha hiyo kuna wakali wengine wanaopewa nafasi ya kutamba. Kiungo Oscar wa Brazil naye anawekwa kwenye kundi hilo kwa kuwa anaaminika ni kiungo mwenye nafasi kubwa ya kutamba kwa upande wa wenyeji katika michuano hiyo.
Wengine ni winga wa Argentina, Angel Di Maria, staa ambaye alikuwa na msimu mzuri sana klabuni Real Madrid, huku kiungo wa Ujerumani, Toni Kroos atakuwa nafasi ya kutamba na kuwania nafasi ya kutajwa kuwa mchezaji bora wa michuano.