Brazil, Croatia mwanzo wa utamu Kombe la Dunia 2014

Muktasari:
Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari atakuwa ni mwenye furaha kwani ana nafasi ya kukitumia kikosi kilichowaangamiza mabingwa wa dunia Hispania kwa mabao 3-0 katika mechi ya Kombe la Mashirikisho mwaka jana huku nyota wa Barcelona, Neymar akiwa nguvu muhimu ya kikosi hicho.
BRAZIL imepania kutuma salamu za nguvu katika mechi yao ya ufunguzi ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Croatia, leo Alhamisi.
Hali hiyo inatokana na presha za hali ya juu zilizoonekana wakati wa maandalizi ya timu hiyo kwa ajili ya fainali hizo ambazo Brazil ni mwenyeji.
Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari atakuwa ni mwenye furaha kwani ana nafasi ya kukitumia kikosi kilichowaangamiza mabingwa wa dunia Hispania kwa mabao 3-0 katika mechi ya Kombe la Mashirikisho mwaka jana huku nyota wa Barcelona, Neymar akiwa nguvu muhimu ya kikosi hicho.
Mabingwa hao mara tano wa dunia wanapewa nafasi kubwa ya kufuzu katika kundi lao bila matatizo ingawa beki wa Barcelona, Dani Alves alikiri kwamba kuna hali ya wasiwasi katika mechi yao ya ufunguzi na wao watakuwa na kazi ya kuondoa hofu hiyo.
"Kila wakati nimekuwa nikisema kwamba kama huna ile hali ya wasiwasi basi huna sifa ya kuwa profesheno, mechi ya ufunguzi ni ngumu na muhimu,'' alisema Alves.
"Pointi tatu zina maana kubwa lakini pia kuna maana kubwa kutuma ujumbe kwa wapinzani wetu, mechi muhimu katika Kombe la Dunia kwa kila mtu ni mechi ya ufunguzi.''
"Ni Alhamisi ndiyo tutaanza kujua kama kila kitu kipo sawa, tunajiamini na tunautaka wakati wa tukio lenyewe. Tunataka kufurahia Kombe la Dunia."
Swali pekee kwa Brazil katika mechi na Croatia ni kuhusu mchezaji Oscar ambaye ameonekana kuwa kivutio na mchezaji mwenzake wa Chelsea, Willian na sasa anawania nafasi kikosi cha kwanza.
Hata hivyo Scolari aliyeiongoza Brazil kutwaa taji la dunia mwaka 2002, katika mechi na Croatia anatarajia kukomaa na fomula iliyomuwezesha kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Serbia bao lililofungwa na Fred.
Mshambuliaji wa akiba wa Brazil, Jo, akizungumza baada ya mazoezi ya juzi Jumanne alisema kwamba hali ni tulivu katika kambi yao lakini wasiwasi wa kawaida unaweza kuwapo muda wa mechi unapokaribia.
"Kwa wakati huu kila mmoja wetu ametulia, tutakapokwenda Sao Paulo na mechi itakapokaribia kutakuwa na hali ya furaha na mshawasha lakini mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia nyumbani itakuwa tofauti na nyingine,'' alisema.
Mshambuliaji mwingine, Bernard alisema ni muhimu kuanza mashindano na ushindi wakati ambao Brazil inawania kulibeba taji la dunia kwa mara ya kwanza katika ardhi ya nyumbani.
Croatia itamkosa mshambuliaji wake anayekipiga Bayern Munich, Mario Mandzukic anayetumikia kadi nyekundu aliyoipata katika mechi dhidi ya Iceland, Novemba mwaka jana.
Lakini timu hiyo inaye kiungo wa Real Madrid, Luka Modric ambaye alisema kwamba nguzo muhimu katika mechi utakuwa ni mpambano wa safu ya kiungo ingawa alikiri kwamba jukumu la kuikabili Brazil katika ardhi yao ni zito.
"Katika hali ya kawaida kila mechi inaamuliwa kwa kuangalia safu ya kiungo, mara kwa mara mshindi ni timu ambayo huwa na kiungo mzuri,'' alisema Modric.
"Natumaini tutaonyesha uwezo wetu na tunaweza kuwafunga Brazil lakini ukweli ni kwamba hilo ni jambo gumu.''
Modric ambaye ndiyo kwanza ametoka kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Real Madrid pia alizungumzia makali ya Neymar anayetajwa na wengi kuwa nguzo ya Brazil.
"Neymar hakuwa na msimu mzuri Barcelona lakini anaichezea Brazil, ni mchezaji tofauti kabisa lakini naamini tutatafuta namna ya kumdhibiti.''
Mechi hiyo itapigwa katika Uwanja wa Corinthians wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 61,600. Ni uwanja ambao ujenzi wake ulichelewa kutokana na matukio ya vifo vya wafanyakazi watatu waliokufa wakiwa katika shughuli za ujenzi.