De Bruyne aaga zake Man City

Muktasari:
- Kiungo huyo Mbelgiji mkataba wake huko Etihad utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, amefunguka na kudai kwamba ataachana na klabu hiyo ya Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO mshambuliaji Kevin De Bruyne amethibitisha kwamba ataachana na Manchester City mwishoni mwa msimu huu baada ya kuwapo kwenye klabu hiyo kwa muongo mmoja.
Kiungo huyo Mbelgiji mkataba wake huko Etihad utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, amefunguka na kudai kwamba ataachana na klabu hiyo ya Ligi Kuu England.
De Bruyne anahesabika kama mmoja wa wachezaji mahiri kabisa kuwahi kutokea kwenye klabu ya Man City, akishinda mataji sita ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na alikuwapo kwenye kikosi kilichonyakua mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja, 2023.
De Bruyne alijiunga na Man City kwa ada ya Pauni 55 milioni, ambayo iliweka rekodi kwenye klabu hiyo wakati huo, aliponaswa kutoka Wolfsburg katika majira ya kiangazi 2015 na amekuwa akifanya kazi kwa mafanikio makubwa chini ya kocha Pep Guardiola.
Utimamu umekuwa tatizo kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 msimu huu, lakini ataondoka kwenye Ligi Kuu England akiwa mmoja wa mastaa matata kabisa kuwahi kucheza kwenye ligi hiyo. De Bruyne ni mshindi mara mbili wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA, aliposhinda 2020 na 2021, lakini alikiri kwamba kila chenye mwanzo kina mwisho.
Aliandika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii kufichua dhamira yake ya kuachana na Man City na kudai kwamba hii ni miezi yake ya mwisho kwenye kikosi hicho cha Etihad.
De Bruyne amekuwa akihusishwa na mpango wa kutimkia Saudi Arabia au Marekani, ambako atakwenda kubamba dili za pesa nyingi. De Bruyne aliitumikia Man City kwenye mechi 413, amefunga mabao 106 na asisti 118.