Prime
Namba zaipa Simba bao 2 dhidi ya Al Masry

Muktasari:
- Hiyo inatokana na kipigo cha mabao 2-0 ilichokubali ugenini katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya michuano hiyo uliochezwa Jumatano iliyopita nchini Misri.
SIMBA ina deni la kurudisha mabao mawili kisha kusaka la ushindi itakapocheza dhidi ya Al Masry ili kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hiyo inatokana na kipigo cha mabao 2-0 ilichokubali ugenini katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya michuano hiyo uliochezwa Jumatano iliyopita nchini Misri.
Kuelekea mchezo huo wa marudiano utakaofanyika Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, takwimu zinaonekana kuibeba Simba katika suala zima la kufunga mabao mawili uwanja wa nyumbani, huku ikiwa na mtihani wa kuwazuia wapinzani wao Al Masry wasifunge kwani nao wana wastani wa kufunga bao moja kwa mechi za ugenini.

Rekodi za Simba wakiwa nyumbani msimu huu wa 2024-25 katika michuano ya CAF, zinaweka matumaini kwa mashabiki wa Msimbazi. Kivipi? katika mechi nne ilizocheza nyumbani hadi sasa, Simba imeshinda zote ikifunga mabao manane na kuruhusu mawili tu.
Septemba 2024, Simba ikiwa nyumbani ilishinda 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli katika mchezo wa marudiano wa raundi ya pili baada ya kutoka 0-0 ugenini. Ushindi huo uliipeleka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika hatua ya makundi, Simba ambayo ilikuwa Kundi A, iliendelea kuwa moto wa kuotea mbali ikiwa nyumbani. Novemba 27 iliwabwaga Bravos do Maquis kwa bao 1-0, kabla ya kuilaza CS Sfaxien kwa mabao 2-1 Desemba 15, 2024. Januari 19, 2025 Wekundu wa Msimbazi waliendeleza ubabe wao kwa kuichapa CS Constantine mabao 2-0.
Kwa ujumla, Simba ina wastani wa kufunga mabao mawili kwa kila mechi ya nyumbani katika mashindano haya msimu huu. Ulinzi wake nao umeimarika, kwani hakuna timu iliyowahi kuifunga zaidi ya bao moja nyumbani.

Hivyo mchezo huu ni fursa kwa Simba kujiuliza kwa kile kilichotokea Misri siku chache zilizopita na kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids anaamini utakuwa mchezo tofauti kabisa na ilivyokuwa ugenini.
“Tayari wenzetu wana mtaji wa mabao hivyo tunatakiwa kufanya zaidi ya ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza hasa katika safu yetu ya ushambuliaji pia kuongeza umakini katika kujilinda,” alisema kocha huyo.
Kwa upande wao, Al Masry ambao walikuwa kundi D, wanakuja Dar es Salaam wakiwa na kumbukumbu chungu za mechi zao za ugenini msimu huu. Katika mechi nne zilizopita za Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa ugenini, hawajawahi kushinda hata mara moja.

Walianza kampeni kwa kupoteza dhidi ya Al Hilal Benghazi kwa mabao 3-2, kabla ya kusonga mbele kwa mikwaju ya penalti 3–5. Katika hatua ya makundi, walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Black Bulls Maputo na Enyimba, kisha kupoteza 1-0 dhidi ya Zamalek.
Kwa ujumla, Al Masry wakiwa ugenini msimu huu katika mechi za kimataifa wamepoteza mechi mbili sawa na sare zao, hawajashinda hata moja. Wameruhusu mabao sita na kufunga manne katika mechi hizo nne, ishara kuwa ulinzi wao ugenini sio thabiti lakini pia wana wastani wa kufunga bao moja.
Kutokana na Simba kuwa na uhitaji wa kufunga mabao 3-0 ili kuvuka kwenda nusu fainali, inabidi wawe makini na Al Masry ambayo licha ya kwamba haina rekodi ya ushindi ugenini msimu huu, lakini inabebwa na uwezo wao wa kufunga angalau bao moja.
Endapo Al Masry wakipata bao moja katika mchezo huo, Simba italazimika kufunga mabao manne ili kusonga mbele vinginevyo bao la ugenini litawatibulia ndoto zao za kufika fainali na hata kuleta taji la kwanza la Afrika kihistoria katika ardhi ya Tanzania.

Akizungumzia ushindi wao katika mchezo wa robo fainali ya kwanza, kocha wa Al Masry, Anis Boujelbene ambaye aliteuliwa kubeba mikoba ya Ali Maher, baada ya kuondoka ES Zarzis ya Tunisia, alisema: “Simba ilitupa upinzani mkubwa katika vipindi vyote, bado tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya kwenye mchezo wa marudiano lakini nashukuru wachezaji wangu kwa kujitoa na mashabiki kwa kuwa nyuma yetu.”