Europa League... Spurs nyumbani, Man United ugenini

Muktasari:
- Fainali ya michuano hiyo itafanyika Bilbao huko Hispania, lakini kabla ya kufika huko ni lazima timu zipigane vikumbo kwenye kusaka tiketi ya fainali, ambapo mechi nne za robo fainali zitapigwa Alhamisi, Aprili 10 kabla ya timu hizo kurudiana Alhamisi ya wiki ijayo, Aprili 17.
MADRID, HISPANIA: MCHAKAMCHAKA chinja ndicho kinachoendelea kwenye mikikimikiki ya Ulaya, ambapo usiku wa Alhamisi zitapigwa mechi nne matata kabisa za kwanza kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya UEFA Europa League.
Fainali ya michuano hiyo itafanyika Bilbao huko Hispania, lakini kabla ya kufika huko ni lazima timu zipigane vikumbo kwenye kusaka tiketi ya fainali, ambapo mechi nne za robo fainali zitapigwa Alhamisi, Aprili 10 kabla ya timu hizo kurudiana Alhamisi ya wiki ijayo, Aprili 17.
Mechi ya mapema kabisa itazikutanisha Bodo/Glimt na Lazio. Kipute hicho kinasubiriwa kwa hamu kuona ni kitu gani kitakachokwenda kutokea, ambapo mabingwa wa Norway, Bodo ni timu hatari kwenye kufunga mabao, ikifanya hivyo mara 24 msimu huu na kuwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi kuliko timu nyingine yoyote kwenye michuano hiyo.
Baada ya mechi hiyo, zitafuatia nyingine tatu zitakazochezwa muda mmoja, ambapo Tottenham Hotspur itakuwa nyumbani kucheza na miamba ya Ujerumani, Eintracht Frankfurt.
Spurs inaamini ubingwa kwenye Europa League ndiyo utakaowapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, hivyo kufikia kwenye hilo inahitaji kufanya vizuri na kushinda kwenye mechi hiyo itakayopigwa London kabla ya kwenda kurudiana huko Ujerumani wiki ijayo.
Timu hizo ziliwahi kukutana kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2022/23, ambapo Spurs ilishinda 3-2 nyumbani baada ya sare ya 0-0 huko Frankfurt.
Wababe wa Scotland, Rangers watakuwa na shughuli pevu mbele ya Athletic Bilbao ya Hispania.
Mechi hiyo inatazamiwa kuwa ya kutafutana uwanjani kwa wachezaji wa timu hizo kutokana na rekodi kuonyesha kwamba zitakutana kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Uefa.
Kwenye historia yao, Rangers na Bilbao hazijawahi kukutana kwenye mechi za kiushindani za michuano ya Uefa, hivyo kila mmoja itahitaji kuanza vyema kwenye kete yao ya kwanza. Itakuwaje?
Lakini, macho na masikio ya wengi yatakuwa huko Ufaransa, ambako Lyon itakuwa nyumbani kukipiga na Manchester United.
Lyon inaonekana kuichukulia michuano hiyo siriazi sana msimu huu baada ya kushinda kwa jumla ya mabao 7-1 dhidi ya FCSB kwenye hatua ya 16 bora.
Mastaa wake Malick Fofana, Georges Mikautadze na Ernest Nuamah kila mmoja alifunga mara mbili na bila shaka watakuwa na maswali mengi kuwauliza mabeki wa Man United uwanjani.
Kwenye mtoano wa raundi ya 16 bora, Man United iliitupa nje Real Sociedad, ambapo kiungo Bruno Fernandes alifunga hat-trick huku Man United ikitinga hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 5-2.
Lyon inakwenda kukutana na timu ya Man United, ambayo msimu huu imeweka rekodi bora ya kumiliki mpira, kuzidi timu zote ikiwa na wastani wa umiliki wa mpira wa 57.5% katika kila mechi iliyocheza kwenye michuano hiyo ya Europa League msimu huu.
Mechi za nusu fainali ya Europa League zitafanyika Mei 1 na Mei 8, wakati fainali yenyewe itakuwa Mei 21.